Moto Uliozuka Hospitalini Wauwa Wagonjwa 21

Moto Uliozuka Hospitalini Wauwa Wagonjwa 21.

WAGONJWA wapatao 20 pamoja na muuguzi wameuawawa baada ya moto mkubwa kuibuka hospitalini katika Jimbo la Janseong nchini Korea Kusini. Moto huo pia umewaacha wagonjwa wengine 6 wakiwa mahututi baada ya moto huo katika hospitali ya Hyosarang iliyoko kilomita 300 kusini mwa Seoul.

Wengi waliofariki dunia kwa ajali hiyo ya moto ni wagonjwa wazee wenye umri kati ya miaka 70 na 80 na wasioweza kutembea, ambao walishindwa kuukimbia moto huo. Maofisa walisema kuwa wengi waliokufa walikosa hewa kutokana na gesi zenye sumu.

Hata hivyo moto huo ulizimwa kwa takribani nusu saa baada ya vikosi vya kupambana na majanga ya moto kuwasili eneo la tukio. Moto huo ulianza muda mfupi tu baada ya saa sita usiku katika jumba lenye orofa tatu.

Vyombo vya habari vinaarifu kuwa wengi wa wagonjwa waliokuwa katika orofa ya juu ya jumba hilo walishindwa kujiokoa kwa sababu vyuba vyao vilikuwa vimejaa moshi uliotokana na moto. Muuguzi huyo aliyekufa alikuwa akijaribu kuzima moto.

Ripoti ya shirika la Yonhap ilisema kuwa polisi walisema kuwa jumba hilo lilikuwa limefanyiwa uchunguzi wa kiusalama majuzi. Mkurugenzi wa hospitali hiyo Lee Hyung Seok aliomba msamaha na kuwaambia wanahabari kuwa alikuwa ametenda dhambi kubwa, na kuwa hangetoa visababu wakati watu wameaga dunia.

Tukio hili limekuja wakati wananchi wa Korea Kusini wakiendelea kuomboleza vifo vya zaidi ya watu 300 waliofariki katika ajali ya feri iliyotokea mwezi uliopita. Rais wa taifa hilo Park Geung-Hye ameliomba taifa radhi rasmi kwa ajali hiyo ya feri, huku akiahidi kuimarisha viwango vya usalama.

Waziri Mkuu Chung Hong-won wakati huo alijiuzulu kwa madai ya jinsi Serikali ilivyoshindwa kukabiliana na majanga. Ajali hiyo ya hospitali pia imetokea siku moja tu baada ya watu 7 kuuwawa na wengine 20 kujeruhiwa katika mkasa wa moto uliozuka katika kituo cha mabasi jijini Goyang.
-BBC