Na Florah Temba
WANANCHI 81,769 wa kata 12 za maeneo ya tambarare wilaya ya moshi mkoani Kilimanjaro wanakabiliwa na tatizo la Njaa kutokana na Ukame uliosababishwa na upungufu wa mvua katika kipindi cha masika.
Kufuatia hali hiyo wananchi hao wanahitaji chakula cha msaada tani 14,634.6 ili kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeonekana kuathiri shughuli za kimaendeleo.
Hayo yalibainishwa na mkuu wa wilaya ya moshi Bw.Ibrahim Msengi wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na hali ya chakula katika wilaya hiyo.
Alisema chakula hicho kinahitajika kuanzia sasa kutokana na kwamba katika msimu wa masika mvua zilikuwa chache hivyo maeneo ya tambarare hayakupata kitu.
Alisema tayari wameshafanya tathmini ili kutambua maeneo ambayo yaliathirika zaidi na tatizo hilo ambapo chakula kinachohitajika zaidi ni mahindi kutokana na kwamba zao hilo hulimwa kwa wingi maeneo ya tambarare.
Kutokana na hali hiyo Bw. Msengi alisema kwa sasa kuna haja ya Wananchi kubadilika na kuanza kilimo cha Mazao yanayohimili ukame, hatua ambayo itasaidia kukabiliana na tatizo hilo ambalo limeikabili Wilaya hiyo kwa muda mrefu sasa.
Alisema endapo wananchi wataelimishwa na kuhamasishwa kulima Mazao yanayostahimili Ukame kama Mtama,mihogo pamoja na viazi hali hiyo itakuwa tofauti na tatizo la njaa litapungua kama si kuisha kabisa.
“Kwa sasa zaidi ya tani 14,634.6 za chakula zinahitajika katika maeneo ya tambarare ili kunusuru hali iliyopo kwa hivi sasa na hali hiyo imekuwa ikiathiri kwa kiasi kikubwa wanafunzi na kuchangia kiwango cha Taaluma kuporomoka kwani Wanafunzi hutoroka mashuleni kwenda kutafuta Chakula manyumbani kutokana na shule nyingi kukosa chakula cha mchana”alisema Bw. Msengi.
Hata hivyo alishauri Wananchi wa Wilaya hiyo ambao walifanikiwa kupata Chakula kukitumia vizuri hadi msimu ujao wa Mvua za vuli kwa kuwa hali ya Chakuli si nzuri na kwamba mahitaji ya Chakula yanaweza kubadilika na kuongezeka endapo hali ya Ukame itaendelea .