MGOMO wa madaktari umezidi kutikisa na kuathiri huduma za afya katika hospitali kuu nchini, huku Taasisi ya Mifupa (Moi) ikitangaza rasmi kufunga kliniki zote zinazohudumia wagonjwa wa nje hadi mgomo huo utakapomalizika. Mkurugenzi Mtendaji wa Moi, Profesa Lawrence Museru alitangaza uamuzi huo wa kufunga huduma hizo jana, akisema taasisi hiyo ina madaktari bingwa 30 pekee na ndiyo wanaofanya kazi huku madaktari wake wengine zaidi ya 30 wakiwa kwenye mgomo.
Alisema kufuatia hatua hiyo, madaktari waliobaki hawawezi kujigawa na kuhudumia wagonjwa wote wanaofika katika taasisi hiyo na ndiyo sababu, wamelazimika kusitisha huduma kwa kliniki.
“Baadhi ya madaktari wapo kwenye masomo, waliopo kwa sasa ni 60 na kati yao 30 wapo kwenye mgomo hali hii imetulazimu kusitisha huduma hizo ili hizi nyingine zitolewe kwa ufanisi,” alisema Profsea Museru.
Alisema hali hiyo pia iliangalia aina ya madaktari waliopo na kwa sasa itawalazimu kuwatumia madaktari hao katika mambo mengine ambayo awali, walikuwa hawayafanyii kazi.
Wanajeshi watua
Katika hali ambayo haikutarajiwa, mgonjwa Fatuma Mohamed, Mkazi wa Upanga, Dar es Salaam aliyefika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jana alimwambia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda aangalie maslahi ya umma kwa kuzingatia matatizo ya walio wengi.
Alisema hayo baada ya kumsikiliza Dk Mponda akiwataka wagonjwa kurejea katika hospitali hiyo kwa madai kuwa huduma zipo.
Dk Mponda alifanya ziara hospitalini hapo jana na baadaye akawa anatoa maelezo kwa waandishi habari akiwataka waandike habari za kuhamasisha wagonjwa kufika MNH na kwamba baadhi ya huduma zinaendelea kama kawaida.
Mgonjwa huyo ambaye alijichomeka katikati ya msafara wa waandishi hadi chumba cha mkutano uliofanyika Moi, alipingana na maelezo ya waziri huyo na kumhoji vipi anasema huduma zipo wakati yeye anaumwa na aliambiwa aende nyumbani, hadi hapo atakapotangaziwa kurejea upya kwa huduma.
“Mheshimiwa Waziri mimi si mwandishi wa habari ni mgonjwa, unaposema tuwashawishi wagonjwa waje kutibiwa Muhimbili mbona mimi nimekuja na kuambiwa niondoke hadi nitakapoambiwa hali imetengamaa? Sasa tutawezaje kuwashawishi wengine?”
Akijibu swali hilo Waziri alisema katika baadhi ya maeneo, madaktari wanafanya kazi na kwamba Serikali inaendelea na utaratibu wa kuhakikisha kuwa katika maeneo mengine huduma zinarejea kwenye hali yake ya kawaida pia.
Katika kukabiliana na mgomo huo, jana madaktari 15 kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliwasili Muhimbili kuanza kazi.
Timu hiyo ya wanajeshi iliyoongozwa na Brigedia Jenerali Dk Luhindi Msangi imepangiwa kufanya kazi katika kitengo cha kuhudumia wagonjwa wa dharura ambako uongozi ulikiri huduma zake zilizorota zaidi.
Burigedia Jenerali Dk Msangi aliwaambia waandishi wa habari kwamba ingawa wamefika katika eneo hilo kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kuziba pengo la madaktari walio kwenye mgomo, bado wamelazimika kujigawa kwa kuwa maeneo wanakotoka kunahitaji la madaktari pia
Ilivyokuwa jana
Katika Hospitali ya Temeke, mgomo wa chinichini uliendelea. Mmoja wa wagonjwa, Florence Kilio alisema kwamba alifika hospitalini hapo kumuona daktari lakini akaambiwa asubiri hadi saa nane mchana.
Hali katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando imezidi kuwa mbaya. Wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo wameitaka Serikali kumaliza tofauti zake na madaktari hao haraka ili kuokoa maisha yao.
Akizungumzia hali hiyo, Waziri Saidi anayemuuguza baba yake, Saidi Kaombwe (76) katika chumba cha wagonjwa mahututi namba E703, alisema madaktari walipita jana kwa mara ya kwanza tangu kuanza mgomo, lakini kwa kile alichokiita kuwa ni kiujanja ujanja.
Waziri ambaye yuko hospitalini hapo tangu Desemba 30, mwaka jana alisema licha ya madaktari kuonekana kama wako kazini lakini hali halisi ni kwamba hakuna chochote kinachofanyika kwa mgonjwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Charles Majinge alisema kwa ujumla hali hospitalini hapo si nzuri: “Nina orodha ya madaktari bingwa wanafunzi 16 ambao nimeandika barua kwenda chuoni ili waweze kuchukuliwa hatua,” alisema Majinge.
Dk Majinge alisema mbali na madaktari hao kuwa vinara wa mgomo huo, pia wamekuwa wakifanya vitisho kwa madaktari wengine ili wagome na kuwatisha wagonjwa wasitoe taarifa yoyote kwa uongozi wa hospitali hiyo.
Askofu Mkuu wa huduma ya Good News For All Ministry, Charles Gadi ameitaka Serikali kutenga mpango wa muda mfupi ili kushughulikia matatizo ya madaktari na wauguzi.
Akizungumza jana mara baada ya kutembelea Muhimbili na kuwaombea wagonjwa, Askofu Gadi alisema Serikali ndiyo yenye uwezo wa kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya afya nchini:
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema haikutakiwa kutumia ubabe kuwarejesha madaktari kazini.
Alisema watumishi wa sekta ya afya nchini ni wachache kinyume na utaratibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), linalomtaka daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 10,000.
“Taarifa zinaonyesha daktari moja wa Tanzania anapaswa kuhudumia wagonjwa 28,571 wakati WHO limeweka kiwango cha daktari mmoja kuhudumia watu 10,000. Hali hii imekuwa ikilalamikiwa na kuchangia kuwepo kwa huduma duni,” alisema Dk Bisimba.
CHANZO: Mwananchi