Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Mobile Connect inayotoa huduma za teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kutumia simu za mkononi wamezindua huduma mpya inayoitwa SMS Tafsiri. Akizungumza katika ofisi zao zilizopo Mikocheni jijini Dar es Salaam, Meneja wa Huduma hiyo, Bi. Teddy Qirtu alisema inalenga kusaidia watu kunufaika na simu za mkononi zaidi ya kuzungumza, kutuma ujumbe mfupi na kupata huduma za kibenki.
“Huduma hii ni ya kwanza kufanyika katika ukanda huu. Tumeianzisha kwa sababu tunaamini watu wengi wanapata changamoto ya kutaka kujua tafsiri ya neno au maneno katika nyakati tofauti kwa mfano wakati wa maongezi, katika kujaza fomu mbalimbali au kuandika barua”, alisema.
Alisema huduma ya SMS Tafsiri inayotumia lugha 15, inalenga kutoa ufumbuzi wa haraka, wakati wowote na mahali popote juu ya changamoto hizi kwa jamii. “Hivi sasa huduma ya SMS Tafsiri inatumia Kiswahili, Kiingereza, Kiarabu, Kichina, Kijerumani, Kifaransa, Kihindi, Kijapani, Kilatino, Kihispania, Kirusi, Kituruki, Kiebrania, Kiitaliano na Kiswidi,” alisema Bi. Qirtu.
Akifafanua kuhusu matumizi ya huduma hiyo, Mtaalamu wa Mifumo ya Kompyuta wa kampuni hiyo, Emmanuel Kagongo alisema huduma ya SMS Tafsiri ina sehemu kuu tatu ambazo zinamuwezesha mtumiaji wa simu kutafsiri neno (word), kutafsiri sentensi (phrase) na kutambua lugha iliyotumika katika maandishi.
Akitoa mfano wa namna ya kutumia huduma hiyo, alisema mtumiaji anapaswa kutuma ujumbe mfupi wenye neno ‘tafsiri’ au ‘translate’ kwenda namba 15564 kwa kufuata maelekezo yaliyoainishwa.
“Kwa mfano, ili kutafsiri neno: Andika ujumbe ukiwa na neno la kwanza “Tafsiri” au “Translate”, acha nafasi, andika neno unalotaka kutafsiri, weka alama ya mkato, andika lugha ya kwanza, weka alama ya mkato, andika lugha unayotaka kutafsiriwa. Kisha tuma ujumbe wako kwenda namba 15564, na utapata maana ya ulichouliza kupitia SMS,” alisema.
”Ili kutafsiri sentensi, Kagongo alisema: unaandika ujumbe mfupi ukiwa na neno la kwanza “Tafsiri” au “Translate”, acha nafasi, andika sentensi unayotaka kutafsiri, weka alama ya mkato, andika lugha ya kwanza, weka alama ya mkato, andika lugha unayotaka kutafsiriwa. Kisha tuma ujumbe kwenda namba 15564.
Alisema taarifa zaidi za huduma hiyo zinapatikana kwenye tovuti ya www.mconnect.co.tz na kwamba kila ujumbe utatozwa sh. 250/-.