Mfanyabiashara maarufu ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akitembea kwenye ‘Red Carpet’ mara baada ya kuwasili katika hotel ya Hilton Sandton jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwenye hafla ya utoaji tuzo iliyoandaliwa na jarida maarufu la Forbes na kutunukiwa tuzo ya “Forbes Africa Person Of the Year 2015”.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog).
Na Modewjiblog team
MFANYABIASHARA na mtu mwenye taasisi ya kusaidia jamii, Mohammed Dewji maarufu kama Mo ametunukiwa tuzo ya jarida maarufu la Forbes ya “Forbes Africa Person Of the Year 2015” katika hafla iliyofanyika Novemba 27 mwaka huu jijini Johannesburg, Afrika Kusini.
Mfanyabiashara huyo pia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya Mohammed Enterprises T Ltd (MeTL Group) kampuni iliyoanzishwa na na baba yake katika miaka ya 1970 ambayo sasa imekua na kujikita katika viwanda vya nguo, usagaji nafaka, utengenezaji wa vinywaji baridi, usindikaji wa mafuta ya kula, usindikaji wa chai na kuendesha mashamba ya mkonge ambapo tayari anashea ya asilimia 40 ya soko.
Mo ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda watu watano mashuhuri barani Afrika. Watu hao ni Nkosazana Dlamini Zuma, mke wa Kwanza wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma. Mama huyo kwa sasa ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU). Mwingine ni Rais wa sasa wa Nigeria, Muhammadu Buhari aliyetambuliwa kutokana na kuanzisha vita dhidi ya rushwa nchini mwake.
Aidha wapo Arumna Otei, mchumi mahiri raia wa Nigeria ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia. Pia alikuwemo Mwandishi maarufu wa vitabu wa Nigeria, Chimanda Ngozi Adichie ambaye moja ya vitabu vyake vinaelezea picha halisi ya Afrika inavyofikiriwa duniani.
Akitoa neno la shukurani baada ya kukabidhiwa kwa tuzo hiyo Mo, alisema anatoa tuzo hiyo kwa vijana wa Kitanzania kwani ndio nguvu kazi inayobeba uchumi wa nchi.
Mo ambaye kampuni yake ya MeTL inaongoza kwa kutoa ajira nchini, ikiwa imetoa ajira 26,000 kote katika viwanda vyake 31 vilivyopo nchini na katika mataifa matano ya Afrika, alisema amefurahishwa na tuzo hiyo ambayo anaitoa kwa vijana kwa kutambua pia wajibu mkubwa walionao katika kukabiliana na umaskini.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akifurahi jambo na baadhi ya wageni waalikwa nje ya ukumbi wa hafla hiyo ya utoaji tuzo iliyoandaliwa na jarida la Forbes.
Alisema ajira 26,000 zimegusa watu wengi nchini na kwamba ana matumaini makubwa ya siku za usoni kutoa ajira zaidi kutokana na biashara zake kuendelea kukua.
“Heshima yangu kubwa haitokani na utajiri, maana kama utajiri wako hauna msaada wala kugusa watu masikini hauna maana yeyote, hivyo basi heshima hii ni kutokana na kwanza bidhaa zangu kugusa maisha ya watu kila siku kuanzia sukari na majani ya chai asubuhi pamoja na unga wa ngano, lakini pia chakula cha mchana kwa unga wa sembe, mafuta ya kupikia na maji ya kunywa, bidhaa zote hizo za Mohammed Enterprises zinagusa maisha kila nyakati katika siku.
“Nina viwanda 31 ambavyo vimekuwa vikitengeneza bidhaa za Kitanzania na kuziuza kwa Watanzania kwa bei yenye unafuu mkubwa, mathalani tunauza maji kwa bei chini ya dola moja kwa shilingi za Kitanzania 200, hakuna hata Ulaya, nina kiwanda cha khanga na vitenge ambacho malighafi zake zote ni za Kitanzania, hivyo kuna kusaidia serikali kwa kulipa kodi ipasavyo, lakini pia kusaidia moja kwa moja ajira za Watanzania walio wengi ambao tatizo lao kubwa katika kundi la vijana ni ajira”
Alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza baba yake kwa kumwita mjasiriamali shujaa ambaye alitoka kuanzia dereva wa malori baada ya kuhitimu kidato cha nne mwishoni mwa miaka ya 1960 hadi kufikia ubilionea. Alisema alipata maono ya utajiri hasa kutoka kwa baba yake huyo aliyekuwa akimshirikisha biashara tangu akiwa mdogo.
“Mwanaume mwenye ndoto huhitaji mwanamke mwenye maono. Na nimebarikiwa mwanamke ambaye kwa miaka 15 amekuwa akinipa sapoti isiyoyumba.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akibadilishana ‘Business card’ na mmoja wa wageni waalikwa katika hafla hiyo.
“Saira, nina shukurani nyingi kwako kwa kuwa nguzo ya familia yetu, mama wa heshima kwa watoto wetu watatu,” alisema Mo kwenye hafla hiyo.
Kwa utulivu, Mo alisema: “Baba, zawadi kubwa ambayo ulinipa katika maisha yangu ni muda wako, na kwa hilo nitakuwa mwenye deni la shukurani kwako siku zote za maisha yangu.”
Mo ambaye moyo wake wa binadamu ulimfanya awanie uwakilishi Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kushinda nafasi hiyo na hivyo kuwawakilisha wanasingida kuanzia 2005 na 2015 amesema maisha ni changamoto kubwa inayobadilishwa kwa utumishi wenye nia ya dhati kwa umma.
Alisema alipowania uwakilishi alikuwa na sababu: “Nilikuwa na umri wa miaka 24, nilikwenda Singida kutoa heshima kwenye kaburi la marehemu babu yangu. Sikuwa nimefika huko tangu nilipoondoka nikiwa na umri wa miaka mitatu.
“Nilipokuwa njiani, nilimuona mzee akiwa na maji yenye rangi ya njano, machafu ambayo aliyatumia kwa kunywa. Nilishangaa, maana hali ile sikuwahi kufikiri kama ipo vile. Kipindi hicho nilikuwa nimemaliza Chuo Kikuu cha Georgetown, Marekani.”
Mo anasema kuwa aliingiwa na hisia kutaka kujua nini hasa alichokuwa anahitajika kufanya, alimfuata yule mzee aliyekuwa na maji yale, alipozungumza naye, aliwazungukia watu wengine na kuridhika kuwa ile ndiyo hali halisi, hapo ndipo fikra ya kwa nini agombee ubunge ilipoanzia.
Anasema kuwa baada ya kujiridhisha hivyo, alirudi kwa mzee wa kwanza, alizungumza naye na kumuuliza ni kwa nini shida ile ilikuwa haizungumzwi kwa upana katika mamlaka husika.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji pamoja na ujumbe wake alioambatana nao kutoka Tanzania.
“Nilipojitambulisha yule mzee alisema anamkumbuka babu yangu, kisha akanishauri nigombee ubunge, alinisisitiza mno ili nisaidie kuondoa lile tatizo la watu wa Singida kunywa maji machafu,” alisema Mo.
Anaeleza kuwa alipokuwa njiani kurejea Dar es Salaam, alilifikiria tatizo hilo kwa mapana zaidi, akalifanyia utafiti na kubaini kwamba katika kila watu 10, watatu walikuwa wakipoteza maisha kutokana na maradhi yanayosababishwa na maji machafu.
Anaendelea kusema kuwa aligundua kuwa Singida kulikuwa na tatizo kali la maji safi na salama. Anasema kuwa alibaini uwepo wa tatizo la elimu kuhusu matatizo ya maji.
Jambo lingine ambalo anasema aliligundua ni uwepo wa tatizo la huduma za afya. “Niliwafikiria watoto wangu, jinsi ninavyowapenda, na namna ambavyo kila mzazi anavyompenda mwanaye. Nilipingana na hali kuwa watoto wa Uingereza na Marekani wamependelewa zaidi. Maisha ni sawa bila kujali chochote,” anasema Mo.
Sehemu ya ujumbe kutoka Tanzania uliombatana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji kwenye hafla hiyo.
“Niliona lazima nitimize wajibu wangu. Kutimiza malengo yangu ya kusaidia jamii, kufanikiwa katika biashara. Mambo hayo mawili hisani na biashara nimeyaweka pamoja na ndiyo maana nimefika hapa leo, tunajivunia sana kuitwa METL nembo ya Watu. Katika miaka yangu 10 kama mbunge, nimefanya mabadiliko mengi. Nilikuwa na sababu ya kupata mkopo nafuu wa dola milioni 35, ambao ulisababisha kuwekwa kwa miundombinu ya maji safi na salama Manispaa ya Singida.
“Niliitumia MeTL, tuliweza kudhamini shughuli nyingi za maendeleo ya kijamii. Kuhusu elimu, nilifanikisha kujenga shule 15, zikawa 17, kabla ya hapo tulikuwa na shule mbili tu. “Kuhusu huduma za afya, hapa nimshukuru mke wangu kwa jitihada zake. Alikuwa Mwenyekiti wa taasisi ya Tumaini la Maisha ambayo imekuwa ikisaidia watu wengi, hasa watoto dhidi ya maradhi ya saratani.”
Burudani mbalimbali zikiendelea ukumbini hapo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Jarida la Forbes Afrika, Sid Wahi akitoa neno la ukaribisho kwa wageni waalikwa. Kulia ni Head of Events wa ABN Productions, Alexander Leibner.
Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania na Afisa Mtendaji Mkuu wa Makampuni ya MeTL Group, Mohammed Dewji akitoa neno la shukurani baada ya kukabidhiwa kwa tuzo, alisema anatoa tuzo hiyo kwa vijana wa Kitanzania kwani ndio nguvu kazi inayobeba uchumi wa nchi.
MO akiteta jambo na Mchumi mahiri raia wa Nigeria ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Arunma Oteh (kulia) ambaye walikuwa pamoja kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo hiyo ambapo pia alimpongeza sana.
Pichani juu na chini MO akiendelea kupongezwa na wadau mbalimbali walioalikwa kwenye hafla hiyo.
Pongezi kwa MO zikiendelea kutolewa.
MO katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Jaguar Land Rover ambao ni miongoni mwa wadhamini wa sherehe za tuzo hizo.
MO katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa Makampuni ya MeTL Group, Vipul Kakad mara baada ya kutwaa tuzo hiyo.
Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Jaguar Land Rover ya Afrika Kusini wakipozi kwenye ‘Red Carpet’.