Mnyika azungumzia kutimuliwa kwa wafanyabiashara Ubungo

Mbunge wa Ubungo, John Mnyika

BAADA ya kuwasikiliza wafanyabiashara ndogondogo zaidi ya 500 walioondolewa kwenye kata ya Ubungo niliwaeleza kuwa kazi ya mbunge ni kuwakilisha wananchi, kuisimamia serikali na kutunga sheria. Nilianza kwa kuwaeleza wazi kwamba siungi mkono biashara kufanyika katika maeneo hatarishi na maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.

Matatizo ya wafanyabiashara ndogondogo katika Jiji na Dar es salaam ni maeneo mengine ya mijini nchini ni ya muda mrefu. Mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni aliahidi kwamba serikali yake ingeyapatia ufumbuzi wa haraka, hata hivyo Oktoba 2006 mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa baada ya kushughulikia msingi wa matatizo aliongoza uamuzi wa siasa kanyaboya wa kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo kinyume na alichowaahidi wakati wa uchaguzi.
Maelezo aliyoyatoa Rais Kikwete wakati huo ni kuwa tunawaondoa maeneo yasiyorasmi ili kuwapeleka kwenye maeneo rasmi muweze kupata anuani, mafunzo na mitaji; ahadi ambayo haijatekelezwa kwa ukamilifu.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli sasa kuwa wafanyabiashara walioondolewa Ubungo waende Machinga Complex suala ambalo nalo ni propaganda kanyaboya kwa kuwa anafahamu kuwa eneo hilo lina uwezo wa kubeba wafanyabiashara takribani 4,500 wakati ambapo wafanyabiashara ndogo ndogo katika mkoa wa Dar es salaam walio katika maeneo kinyume cha sheria ni zaidi ya 150,000. Hivyo, Mkuu wa Mkoa anapaswa kuonyesha mfano wa kuwapeleka wafanyabiashara ndogondogo waliombele ya ofisi yake na maeneo jirani katika Machinga Complex, ambao pekee watajaza. Nimewaeleza kwamba kama suala ni kuvutia wafanyabiashara ili soko lizoeleke watekeleze ushauri niliowapa kwenye vikao husika wa kuongeza ruti za daladala kupitia eneo husika watoe likizo ya kodi kwa wafanyabiashara ndogondogo kwa muda maalum katika jengo husika kama inavyofanya kwa wafanyabiashara wakubwa kutoka nje wanapokuja kuwekeza nchini.

Nikawaeleza kwamba nilitarajia serikali iweke mkazo katika kukabiliana na vyanzo vya mgogoro wa muda mrefu katika serikali na wafanyabiashara ndogondogo badala ya kujikita katika kushughulikia matokeo pekee. Wafanyabiashara ndogondogo wajaibuka ghafla katika eneo la Ubungo, walianza taratibu huku serikali ikiwaachia na hata kuwatambua kwa njia mbalimbali; hivyo kuwaondoa lazima kutanguliwa na maandalizi ya maeneo mbadala ya kufanyia biashara.

Aidha, wananchi kufanyia biashara katika maeneo yasiyorasmi ni matokeo ya udhaifu wa muda mrefu wa serikali wa mipango miji na kushindwa kutenga maeneo ya biashara na kuuza kinyemela maeneo machache yaliyotengwa kwa huduma za msingi za kijamii. Hivyo, uamuzi wa kufungua ukurasa mpya kurekebisha hali hiyo lazima uambatane na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na huduma nyingine za msingi za kijamii.

Serikali ina wajibu huo pamoja na kuwa biashara inaweza kutazamwa kuwa ni suala la mtu binafsi kwa kuwa wanunuzi wa biashara hizo ni wananchi hususani wa kipato cha chini na hali hii ya kuongezeka kwa uchuuji ni sehemu ya athari za kupungua kwa uzalishaji nchini.

Hali ya taifa ya kiuchumi na kijamii ni chimbuko la ongezeko la wafanyabiashara ndogondogo Jijini Dar es salaam, mathalani kasi ndogo ya ukuaji wa ajira hasa katika viwanda na kilimo ikilinganishwa na idadi kubwa ya vijana wanaohitimu shule na vyuo; biashara hizo ni sehemu ya jitihada za vijana wenyewe ‘kujiajiri’ hivyo kuwaondoa bila mfumo mbadala ni kuchangia katika umaskini.

Hivyo; kutokana na hali hiyo nilitoa mwito kwao tuunganishe nguvu ya pamoja kwa kutumia ibara ya 8 na 63 za katiba kuisimamia serikali ili kuhakikisha wanapata maeneo mbadala ya kuendelea na biashara zao kwa: Ni hatua zipi nimetaka zichukuliwe? Unaweza kuzisoma katika: http://mnyika.blogspot.com/2012/04/matokeo-ya-mkutano-wa-mbunge-na.html