MBUNGE wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema Serikali ina kila sababu ya kuwajibika kutokana na mgawo wa umeme unaoendelea kwani majibu yake juu ya mgawo huo yamekuwa ya kujikanganya yenyewe.
Mbunge huyo katika taarifa yake aliyouandikia mtandao huu alieleza kuwa maelezo yanayotolewa na Serikali kuwa mgawo huu umesababishwa na mitambo ya IPTL kuzalisha MW 10 badala ya MW 100 kutokana na upungufu wa mafuta mazito (HFO) yanatosha kwa serikali kuwajibika kutokana uzembe wenye kulitia hasara taifa kwa sababu suala hili lilikuwa likijulikana kwa miezi mingi bila hatua stahili kuchukuliwa.
Aidha Serikali ieleze ukweli kwamba Waziri Ngeleja alitoa kauli potofu bungeni tarehe 15 Februari na Rais Kikwete alitoa ahadi hewa kupitia Hotuba yake kwa Taifa tarehe 1 Aprili kuhusu ukodishwaji wa mitambo ya MW 260 kwa ajili ya umeme wa dharura kuanzia mwezi Julai.