MMILIKI wa Kampuni ya LUGUMI ENTERPRISES LTD, Said Lugumi (MD) amejitokeza kuzungumza na wanahabari huku akidai kazi aliyopewa na Jeshi la Polisi ameikamilisha kwa zaidi ya asilimia 99, tofauti na inavyoelezwa hivyo ameshauri kama anakosa juu ya kazi aliyofanya akamatwe na Jeshi hilo. Zaidi soma hapa taarifa nzima ya mmiliki huyo wa Lugumi akizungumzia tuhuma dhidi yake.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
NDUGU waandishi wa habari, nimewaita hapa leo ili niweze kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa kwa niaba ya Kampuni yetu ya LUGUMI ENTERPRISES LTD, kwa siku kadhaa kumekuwa na habari mbali mbali za kuchafua na kudhalilisha Kampuni yetu pamoja na Mimi Said Lugumi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu.
Nitafafanua mambo yafuatayo kama majibu ya kadhia ambayo sisi na Washirika wenzetu katika shughuli zetu za kibiashara tumekutana nayo,
Kampuni ya LUGUMI ENTERPRISES LTD ilipewa zabuni ya kufunga na kusambaza mitambo ya kuhakiki alama za vidole mnamo mwaka 2011 na kazi tuliifanya kwa kushirikiana na Washirika wenzetu wa kibiashara nje ya Nchi Kampuni za BIOMETRICA LLC (USA) na BIOLINK (RUSSIA), tumefanikiwa kufunga na kusambaza mfumo wa alama za vidole (AUTOMATED FINGER PRINTS IDENTIFICATION SYSTEM – AFIS ) katika maeneo yote ya Nchi yetu na kwa uadilifu kama ambavyo mkataba ulivyohitaji.
Pamoja na kashfa nyingi dhidi ya Kampuni yetu na hususan Mimi binafsi, ukweli ni kwamba hakuna ufisadi wala wizi uliofanyika katika biashara hii muhimu na ya siri, kazi au biashara zinazohusu mambo ya ndani ya usalama wa Nchi zina mashariti yake na itifaki yake, ndio sababu taarifa hii inakusudia kuwatoa wasiwasi ndugu zetu, marafiki zetu na washirika wenzetu na sio kusema hadharani mienendo ya shughuli na zabuni za kazi za namna hii.
Ni uhakika kwamba Rais wetu Mh Dk. John Pombe Magufuli, amedhiirisha pasipo hofu uwezo wake wa kupambana na ufisadi, wizi, utovu wa nidhamu katika utawala wake, hivyo basi kazi hii niliyoifanya na Jeshi la Polisi inaniweka Mimi na Kampuni yangu kwenye wakati rahisi wa kukamatwa na kuhojiwa juu ya tuhuma za kuibia taasisi iliyopewa mamlaka ya kupambana na uhalifu Nchini, sifikiri wala sidhani kama uhalifu wangu unasubiri Kamati ya Bunge kuthibitishwa, ni rahisi sana kwa Jeshi la Polisi kujua je vifaa hivi viko kwenye vituo vya Polisi au haviko?
Na kama haviko kwanini Kampuni yangu ililipwa? na kama nimelipwa kwa kazi ambayo sikuifanya, wale wote walio husika na mchakato wote wa kuhakiki kuwa kazi imefanyika na kuidhinisha malipo kwa kazi hiyo, wanastahili kuwa wapi?
Ninaona hii ni vita ya kibiashara dhidi ya Kampuni yangu, ndio sababu wengine wanahoji vitu vyepesi visivyo na ufahamu, kuwa imekuwaje mimi kupata kazi kubwa kama hii?
Ndoto yangu katika biashara zangu, hii kazi kwangu bado ni ndogo, nimefika hapa kwa kupitia maisha magumu sana, kuna wakati niliishi bila kula na bila kuwa na kazi, lakini siku zote nimekuwa nikiwaza kufanikiwa katika maisha na hapa nilipofika nimefika kwa sababu ya BIDII, MAARIFA, UTHUBUTU NA UJASIRI na safari yangu ya maisha inakwenda mbele zaidi ya hapa.
Mengi yametajwa kuhusu mahusiano yangu na Mh Riziwan Kikwete na wengine kudai kuwa ni mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya Lugumi.
Ukweli ni kwamba hana hata hisa moja katika biashara zangu ila Riziwan ni rafiki yangu, wengine wanasema kuwa yeye ndio amefanikisha shughuli zangu hizi zote, ukweli ni kwamba sio kweli kama inavyosemwa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti mbali mbali, lakini hata kama angekuwa amesaidia kwa namna moja au nyingine kufika hapa nilipo fika kibiashara, je ningekuwa nimevunja utaratibu na sheria za Nchi?
Kwa bahati mbaya katika Nchi yetu shughuli za biashara kubwa zinaonekana kuwa ni za Watu na makundi maalumu na sio za Watanzania kama LUGUMI, ndio sababu hoja zote kwenye mitandao ya Jamii na magazeti zinahoji ninawezaje kufanikiwa katika kiwango hiki wakati Mimi ni Mtoto wa masikini? Jibu ni rahisi, NACHUKIA UMASIKINI.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mh Charles Kitwanga anajua ukweli wa jambo hili, kwani Kampuni yake ya INFOSYS ndiyo ilipewa dhamana kiufundi ya kuunganisha mitambo yote tuliyoisamabaza katika vituo vyote vya Polisi kama tulivyoelekezwa kwenye mkataba na Jeshi la Polisi, Je sio rahisi sana kwa Waziri kulisidia Bunge ili kupunguza gharama za utafiti na kuchafuana kwa kiwango hiki kunako endelea?
Katika Vyombo vya habari mbali mbali imeripotiwa kuwa vituo vilivyofungwa mfumo havizidi kumi na tano, jambo ambalo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) anaweza kuwa na majibu mazuri kuliko Mimi, nawashauri mkamuulize, ila ripoti kutoka ofisini kwetu ambayo imesainiwa na Maafisa mbali mbali waandamizi wa Jeshi la Polisi, inathibitisha kuwa kazi hii imeshafanyika kwa asilimia zaidi ya 99%.
Mwisho, kasi ya Rais wetu katika utumishi wake ni nzuri ila wako Watu wanataka kuitumia vibaya ili kudhalilisha wengine na hatimaye kuwapora haki zao. Tunamuomba Mh Rais awe makini sana katika falsafa yake ya utumbuaji majipu, kwani wengine wanatafuta namna ya kulipa visasi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza
Said Lugumi (MD)
LUGUMI ENTERPRISES LTD