WAKATI Barack Hussein Obama alipotangazwa kama mshindi anayengoja kuapishwa na kuwa Rais wa 44 wa Marekani, niliandika makala, ‘Obama ni Rais wa Marekani si Rais wa Afrika.’
Niliandika hivyo kwa makusudi kutokana na matumaini makubwa, na pengine yanayozidi kawaida walivyokuwa nayo baadhi ya Waafrika kutokana na rangi ya Obama. Nchi jirani ya Kenya (alikotoka Hussein Obama) ilitangaza siku moja rasmi ya mapumziko kusherekea ushindi wa Obama.
Kwa hakika Wakenya hawakujua wanachokisherekea kwani kama ni baraka, basi Obama alikuwa baraka kwa Wamarekani na si kwa Waafrika wala kwa mtu mweusi popote pale alipo hapa duniani.
Baada ya ushindi, ulitokea mjadala mfupi juu ya dini halisi ya Rais Obama, je ni Mkristo ama Mwislamu?
Kwa wale wenye mazoea ya kutambua dini ya mtu kupitia jina lake, basi jina Baraka likanasibishwa na Uislamu na Uafrika jina la Barack likanasibishwa na Ukristo na Uzungu.
Lakini siku zote watu makini tutaendelea kuwatahadharisha wenzetu hawa kwamba dini ya mtu haiko katika jina lake. Si kila aitwaye Abdallah au Mohammed basi ni Mwislamu, wala si kila aitwaye Augustine au Christopher basi ni Mkristo.
Dini ya kweli ya mtu iko moyoni na itathibitishwa na matendo yake na msimamo wake wa kupenda haki na kuchukia dhuluma na uovu.
Maandiko yanasema, “kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele; na fimbo ya Ufalme wako ni fimbo ya adili umependa haki, umechukia maasi (uovu na dhuluma) kwa hiyo Mungu wako amekutia mafuta ya shangwe kupita wenzio,” (hapa msisitizo wangu).
Rais Obama ameonyesha dini yake halisi ya Umarekani. Wanadamu wengi hawajui kwamba Umarekani ni imani ndiyo maana Wamarekani hawaoni haya ‘kumarekanisha’ wanadamu wengine.
Mmarekani yeyote awe Mweupe au Mweusi anaamini juu ya Marekani na anaongozwa na mila hii, ‘nchi yangu kwanza.’ Chini ya mila hii, Mmarekani ataiunga mkono serikali ya nchi yake kwa masuala yote ya nje.
Lakini awapo ndani ya Marekani, anaweza kuipinga Serikali yake, kuikosoa na hata wakati mwingine kuitukana. Mtu ukiangalia jinsi Wamarekani wanavyobishana wao kwa wao, na kushambuliana kwa maneno makali, utadhani wanaweza kuishia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe lakini sivyo.
Mila yao ya ‘my country first’ ndiyo inayowalinda, nchi nyingine ikiiga ni lazima itaishia kushindwa na kuvuna matatizo makubwa.
Upo mfano hai wa nchi ya Kenya enzi za vita baridi kati ya USA na USSR jirani zetu hawa walikuwa ‘highly Americanized’ kiasi cha kutudharau sisi Watanzania.
Hata mfumo wa vyama vingi ulipoingia nchini mwao, Wakenya wakaiga demokrasia ya Marekani, na uhuru walio nao Wamarekani katika kusema mambo ya ndani wawapo ndani ya nchi yao.
Mjadala ulipopamba moto, Rais wa Marekani wa wakati huo George Bush wa pili, alimuuliza Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete wakiwa kwenye mazungumzo ya kawaida.
Rais Bush akasema, ‘hivi kweli ile nchi itapona?’ Akimaanisha kuepuka machafuko, Rais Bush alitishwa na ukali wa mjadala wa mambo ya ndani ya Kenya.
Hayo mazungumzo kati ya Kikwete na Bush yaliwaudhi sana Wakenya, wakailalamikia Tanzania kwa kuzungumzia masuala ya nchi nyingine (yaani Kenya) wakiwa nje ya Tanzania.
Lakini mwisho wa yote kweli Kenya iliingia kwenye machafuko. Wakenya wakachinjana wenyewe kwa wenyewe. Hatimaye Rais Kikwete waliyemlaumu kwamba anazungumza na Bush mambo ya Wakenya badala ya mambo ya Watanzania, akawa ndiye mpatanishi kati ya Raila Odinga na Mwai Kibaki.
Mila ya ‘kumarekanishwa’ haikuwanufaisha Wakenya. Lakini ni Wakenya hao hao walioshangilia ushindi wa Obama kupita kiasi na Serikali yao kutangaza siku rasmi ya mapumziko.
Picha za bibi yake Obama, yaani mama mzazi wa mzee Hussein Obama, zikachapishwa kwenye magazeti mengi wakimnukuu kusema lile au hili.
Lengo halisi la kufanya hivyo lilikuwa ni kuionesha dunia jinsi Rais wa taifa lenye nguvu (Marekani) anavyoungamanishwa na Kenya yao.
Ndipo nilipoandika makala hii kwamba, ‘tusijipe matumaini hewa, Obama ni Rais wa wamarekani siyo Rais wa Waafrika.’ Yawezekana Wakenya wengi walitarajia neema ya aina fulani kutokana na Mjaluo, Obama kuitawala Marekani.
Lakini wakaja kustaajabishwa Rais huyo alipoanza kazi, badala ya Mwai Kibaki wa Kenya kuwa Rais wa kwanza kutoka Afrika kuonana na Obama, akawa Rais Kikwete wa Tanzania. Sijui katika hili walimlaumu nani, Obama au Kikwete?
Neno linalonihuzunisha ni kwamba, Rais Obama anaishambulia Libya, ametuma ndege za kivita zinazojiendesha zenyewe na manowari ziendazo kasi kuibomoa Libya.
Je, marais wa sasa wa Afrika wana msimamo gani? Je, Umoja wa Afrika (AU) una msimamo gani? Na pia wananchi wa kawaida waishio Afrika yaani Waafrika wana msimamo gani? Maana Afrika imevamiwa, Afrika inaharibiwa na wana wa Afrika wanauawa ndani ya bara lao. Je, hii ni jinai ndogo?
Bila shaka mtu anaweza kumuuliza mwandishi, kwani alitarajia Waafrika wanaotawaliwa wafanye nini? Nasema hata kuishabikia tu Marekani ni dhambi.
Kutokana na hayo tunayoyaona kwenye luninga zetu, basi mlalahoi wa kawaida kuishabikia Marekani jinsi inavyomtwanga Kanali Muammar Gaddafi (Rais wa Libya) ni upuuzi uliokithiri.
Ilibidi walau tuonyeshe japo huzuni kwamba bara la Afrika linavamiwa bila kujali kwamba wanaoishi ndani yake ni watu, na hawako duniani kwa bahati mbaya bali ni mwenyezi Mungu alipenda waishi.
Marekani inapotoa maamuzi na kutekeleza kile walichokiamua wao huo Washington, moja kwa moja ni dharau asilimia 100 kwa AU. Marekani imeufanya Umoja wa Afrika kuwa na sifuri ndiyo maana haikutaka hata kuuliza msimamo wa AU.
Nina uhakika endapo ataibuka dikteta kwenye nchi yoyote iliyoko Umoja wa Ulaya (EU), katu Marekani haiwezi kuivamia Ulaya bila ya kushauriana kwanza na EU. Marais wetu wanapodharauliwa, na Umoja wetu (African Union) kuhesabiwa sawa na si kitu, sisi walalahoi tunaishabikia Marekani kwa msingi upi?
Tunafurahia ubabe wake, na uhodari wake katika kuziharibu nchi nyonge? Tukumbuke leo ni Libya, kesho yaweza kuwa Kenya, Tanzania, ama Uganda. Marekani anachokiwinda nchini Libya ni mafuta ya Petroli, anafanya yale yale aliyoifanyia Irak na Saddam Hussein.
Ole kwa nchi za Kiafrika zenye mafuta! Ole kwa ndugu zetu Wapemba, wanaposhangilia utajiri wa mafuta yaliyovumbuliwa, pia watupie macho Irak, Libya na baadaye Saudi Arabia, wakione choyo cha mabeberu, wakae chonjo.
Mtaalamu mmoja aliwahi kusema, mwaka 1982, kwamba mafuta yaliyoko Mashariki ya Kati yanatiririka chini kwa chini, akazitaja nchi za Somalia, Uganda, Tanzania, Zanzibar, na Msumbiji kwamba ziko kwenye mkondo wa mafuta.
Akatabiri kwamba hapo baadaye zitakuja kuwa wazalishaji wapya wa mafuta kwa soko la dunia. Endapo utabiri huu utatimia basi tutarajie mojawapo kati ya haya mawili, la kwanza ni nchi zote zenye mafuta kutawaliwa na marais vibaraka waliosimikwa na Marekani yenyewe. Chini ya Rais kibaraka mambo yale yale ya Jimbo la Ogoni, Nigeria yatajirudia kwenye nchi zetu.
Mafuta yatachimbwa kwa wingi, mazingira yetu ya asili yataharibiwa na utupaji ovyo wa takataka zitokanazo na mafuta, na pia watu wetu wataendelea kuwa maskini wa kutupwa.
La pili linaloweza kutokea ni hili, endapo nchi ya Kiafrika yenye rasilimali ya mafuta itabahatika kupata kiongozi mzalendo na anayependa utajiri wa nchi yake uwanufaishe wananchi wake, basi huyo lazima anyongwe na U.S.A.
Rais mzalendo hatakiwi na wanaoitawala na kuiendesha Marekani, wao wanamtaka kibaraka wa kutii amri zao na maelekezo yao pasipo kuhoji wala kusita.
Jambo la pili linalonihuzunisha kutokana na uvamizi wa Libya, ni huo msimamo wa nchi za Kiarabu chini ya umoja wao ‘The Arab League’. Umeishindwa kuitetea nchi mwanachama wake, na kwahiyo kuleta tafsiri hii kwamba nao umoja wao ni sawa tu na AU, si lolote si chochote.
Ni umoja gani huu unaoshindwa kutetea maslahi na haki za mwanachama wake? Naamini kwa silaha ya mafuta, nchi za kiarabu zingeweza kuugeuza msimamo wa Marekani wa kuvamia mwanachama wao.
Nchi za Kiarabu zingeweza kutoa msimamo wa pamoja kwamba endapo Marekani, Uingereza na Ufaransa zitaivamia Libya, basi nchi za Kiarabu zinavunja uhusiano wa kibalozi na mataifa hayo na pia hazitauza mafuta yake U.S.A, Ufaransa na Uingereza.
Nina uhakika Wamarekani, Wafaransa na Waingereza wangeogopa kupoteza biashara ya mafuta, wasingethubutu kufanya haya tuyaonayo.
Nailaumu AU kwa kupoteza misimamo ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (O.A.U) ya kulinda utambulisho wa Afrika duniani. Nakumbuka mwaka 1967 nchi ya Misri, iliingia kwenye mapigano na nchi ya Israeli. Kwenye vita hiyo iliyopiganwa mfululizo kwa siku sita, nchi ya Israeli iliteka milima ya Golan na Sinai, maeneo ambayo yako ndani ya mipaka ya Misri. O.A.U ilikutana, kutafakari, na kutoa msimamo wa Afrika.
Ikaonekana kwamba Misri iko ndani ya Afrika, na ni mwanachama wa O.A.U, kwahiyo nchi zote za Kiafrika zivunje uhusiano wa kibalozi na Israeli ili iwe ishara kwamba haziafikiani na tendo la Israeli kuyakalia maeneo ya Golan na Sinai.
Lakini huu umoja wa sasa ambao nathubutu kuuita umoja ‘boya’, umeshindwa kuonesha misimamo na pia hauna mikakati yoyote ya kujiimarisha.
Laiti kama AU ingekuwa umoja makini , basi walau ndani ya UN nchi zote za Kiafrika zingeenda na msimamo moja. Hatua kama hiyo hata kama Afrika aina kura ya veto (turufu), bado ingeweza kujiundia veto kwa umoja wake.
Lakini huu umoja dhaifu hauna faida kwa Waafrika wala kwa nchi wanachama ni sawa na mkusanyiko wa watu wafanyao pikiniki.
Mwisho, nichukue nafasi hii kuwatahadharisha wale wanaoendekeza na kuuweka mbele udini, ingekuwa umoja wa nchi za Kiarabu unaongozwa na wenye majina ya Julius, Martin, Christiano, John, Joseph, nakadhalika ingelikuwa nongwa.
Wangeshambuliwa kwa ukatili dhidi ya Waislamu wa Tripoli, Benghazi za maeneo mengineyo. Sasa inapotokea msemaji wa nchi hizo kuwa ni Amir Moussa, inabidi dini iwekwe kando.
Hata hivyo, tunaoujali ukweli na haki tunawasikiliza kwa subira, tusikie wanasemaje kwa uamuzi wa aina hii ambapo mwislamu anaridhia mauaji dhidi ya Waislamu wenzake.