MLINZI mkuu wa zamani wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Peter Bwimbo (87) ameandika kitabu kwa mara ya kwanza akiweka wazi jinsi Mwalimu alivyotoroshwa kutoka katika mikono ya wanajeshi walioasi katika Maasi ya Jeshi ya mwaka 1964.
Kitabu hicho: “ Peter D.M Bwimbo: Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere” kimechapwa mwaka huu nchini na Kampuni ya Mkuki na Nyota na kina jumla ya kurasa 131 zinazoeleza mambo mbalimbali ambayo hayakuwahi kuelezwa waziwazi na yeyote.
Kwa mfano, kitabu hicho; zaidi ya kueleza namna Nyerere alivyotoroshwa –kimeeleza pia namna aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashidi Kawawa, alivyonusurika kufa kwa kuvuta hewa chafu nchini Misri kwenye miaka ya 1960 na namna Mwalimu pia alivyoamua kutopanda ndege iliyokuwa imeandaliwa na mwenyeji wake, aliyekuwa Rais wa Zaire, Mobutu Seseseko, kutokana na hofu za kiserikali.
Ilivyokuwa wakati wa maasi
Januari 20, mwaka 1964, askari wa Kiafrika waliokuwa ndani ya Jeshi la KAR waliasi kwa madai kwamba ingawa Tanganyika ilikuwa imepata Uhuru, bado jeshi hilo lilikuwa chini ya Waingereza na wanajeshi wengine wenye asili ya Kiasia.
Katika kitabu hicho, Bwimbo ameandika kwamba maasi hayo yalitokea ghafla pasipo mipango hiyo kufahamika hata kwa Idara ya Kikachero ya wakati huo (Special Branch) na kwamba wahusika hawakufahamika mapema mpaka walichopanga kilipokamilika na hatimaye maasi kuanza.
Ni maasi hayo ndiyo yaliyosababisha KAR kuvunjwa na hatimaye kuundwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) kama inavyofahamika sasa.
Operesheni Magogoni
Bwimbo anasema katika kitabu hicho kwamba aliipachika kazi ya kumwokoa Mwalimu na Kawawa wasitekwe na waasi waliokuwa wamevamia Ikulu jina la Operesheni Magogoni, kwa vile kivuko kilichotumika kuwaondoa viongozi hao kutoka Ikulu na kuwapeleka Kigamboni kilikuwa kinafahamika kwa jina la Magogoni.
“Nilipigiwa simu majira ya saa 8 usiku na ofisa wa kitengo chetu aliyekuwa mkuu wa zamu usiku huo hapo Ikulu, Leon Kazimili, kwamba kuna taarifa kuwa katika kambi ya Calito (Lugalo) palikuwa na dalili kuonyesha kuwa imevamiwa na majeshi ya kigeni usiku huo; Januari 20, 1964.
“ Niliamka haraka kuelekea Ikulu nikiwa na gari langu kwa sababu Ikulu ndiko mahali walipokuwa Rais pamoja na Waziri Mkuu ambaye nyumba yake ilipakana na Ikulu upande wa Kaskazini. Leon Kazimili sasa ni marehemu. Niliwasili Ikulu kutoka nyumbani kwangu Upanga majira ya saa 8:20 usiku.
Wakati huo, tayari watu wa usalama walikuwa wamewaamsha Rais na Waziri Mkuu kuwaeleza kuhusu kilichotokea Calito.
“ Nilipanga haraka akilini mwangu hatua za kuchukua katika hali ya dharura kama hiyo kutokana na mafunzo niliyokuwa nimeyapata nchini Marekani mwaka 1963. Nilitoka nje ya viwanja vya Ikulu kwa nyuma upande wa baharini kwa miguu kama majira ya saa 8:45 usiku huo nikiwa na Nyerere na Kawawa, bila wasiohusika kufahamu.
“ Mkurugenzi wangu (Mkuu wa Special Branch) pamoja na Kamishina wa Polisi (sasa IGP) walibakia katika eneo la Ikulu. Ni muhimu kupotosha ukweli katika mazingira haya ya dharura ili maadui au wasiohusika wasifahamu kinachoendelea wakati huo.
“ Nilikuwa na askari polisi wawili wenye sare waliokuwa wanalinda uwanja wa Ikulu siku hiyo.
Nilitumia usafiri nilioukuta kwenye kivuko cha serikali cha Magogoni baada ya kuwaeleza wafanyakazi waliokuwa wanaendesha pantone siku hiyo kuwa nilitaka kuwawahisha viongozi hao wawili kwenye kikao maalumu kilichopangwa kufanyika katika Chuo cha Kivukoni.
“ Wafanyakazi hao wawili penye kivuko ambao kutokana na mazingira ya usiku huo sikuweza hata kuchukua majina yao, walikubali kutuvusha baada ya kuona kwa macho yao sura za viongozi hao wawili (Nyerere na Kawawa).
Tulipovuka, tuliwaambia wale wafanyakazi kuwa wasikirudishe kile kivuko Magogoni kwa sababu viongozi wangetaka kurejea Ikulu mara tu baada ya kumalizika kwa kikao chao. Lengo lilikuwa ni kuhakikisha kuwa hata kama maadui wangebaini kuwa Rais na Waziri Mkuu wameondoka, wasingeweza kuja Kigamboni kwa wakati huohuo,” ameandika.
Kwa sababu hakukuwa na maandalizi ya kumpokea Mwalimu na Kawawa, Bwimbo ameandika kwamba ilibidi watembee kwa mguu kutoka Kigamboni hadi katika kijiji cha Salanga katika usiku huo wa manane wa kihistoria na kwamba njiani walikuwa wakitishwa na mbwa kutoka katika nyumba walizokuwa wakizipita.
Bwimbo ambaye anasema alipata mafunzo mbalimbali ya masuala ya ukachero katika nchi za Uingereza na Marekani, alisema alikuwa na lengo la kuwapeleka viongozi hao katika nyumba ya kupumzikia viongozi iliyokuwepo eneo la Mji Mwema lakini sababu kulianza kukucha, waliamua kulala kwenye nyumba ya msamaria mwema, Sultan Kizwezwe, ambaye aliwapokea vema na wala hakuwasaliti kwa adui.
Kitabu hicho kinachopatikana katika duka la Tanzania Publishing House (TPH) lililopo mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam, kimeeleza namna mlinzi huyo alivyokuwa akiwakatia mapapai viongozi hao na kula nao; katika wakati ambapo askari waasi walikuwa wakiwatafuta kwa lengo la kuwadhuru au kuwadhalilisha.
Mzee Kizwezwe sasa ni marehemu na Bwimbo alieleza kuwa ingawa Mwalimu Nyerere alitaka kumjengea nyumba kama shukrani zake kwake; msamaria huyo alikataa zawadi hiyo na badala yake alikubali zawadi ya baiskeli.
Katika wakati huo ambao Mwalimu alikuwa akiishi Salanga, ni kiongozi mmoja tu; aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, hayati Bhoke Munanka, ndiye pekee aliyepata fursa ya kupafahamu alikofichwa Mwalimu na kuzungumza naye.
Kwa mujibu wa mtunzi wa kitabu hicho, kilitakiwa kichapwe mapema kuliko mwaka huu lakini kwa sababu ya unyeti wa taarifa za mwandishi huyo, ilibidi kwanza kihakikiwe na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Kitabu hiki cha Bwimbo ambaye ana asili ya Ukerewe, Mwanza, ni cha kwanza kuandikwa na mtumishi mstaafu wa TISS; mojawapo ya taasisi ambazo usiri ni mojawapo ya sababu za kuwepo kwake.
Kitabu hicho kina simulizi mbalimbali za matukio ya kiusalama ambazo hazikuwahi kuwekwa hadharani; ikiwamo kuhusu siku Bwimbo alipotaka kumpiga Nduli Iddi Amin katika mojawapo ya vikao vya wakuu wa Nchi za Afrika (OAU) kilichofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Baada ya Mwalimu kubaini nia ya Bwimbo kumchapa Iddi Amin, mwalimu alimwambia; “Mbe Petro, acha bwana”.