Mlipuko Arusha; Wasaudia Wanne Mbaroni, FBI Watua Arusha

Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal akimjulia hali Restuta Alex (50), aliyelazwa katika Hospitali ya Mount Meru Arusha, baada ya kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu uliotokea juzi. Kushoto ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa na Kulia ni Mkurugenzi wa Maelezo, Assah Mwambene. Picha ya OMR 

WAKATI maofisa wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (FBI) wametua Arusha, raia wanne wa Saudi Arabia na Watanzania wawili wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika kulipua bomu lililoua watu wawili na kujeruhi wengine 61 wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph Parokia ya Olasiti.
Waliofariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45), mkazi wa Olasiti na James Gabriel (16), ambaye alifariki usiku wa kuamkia jana. Tukio hilo lilitokea wakati Balozi wa Vatican na Mwakilishi wa Papa nchini, Francisco Montecillo Padilla alipokuwa akizindua kanisa hilo.

Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema raia hao wa Saudi Arabia walikamatwa jana asubuhi baada ya tukio wakiwa kwenye gari wakielekea Kenya kupitia Namanga. Mulongo alisema raia hao wa kigeni waliingia nchini Jumamosi iliyopita na siku iliyofuata ndipo kukatokea ulipuaji huo. Alisema lengo la shambulizi hilo lilikuwa kumdhuru Askofu Padilla.

“Mtu ambaye tulimkamata jana (juzi Jumapili) ndiye aliyesaidia kuwapata watu hawa wa Saudi Arabia na Watanzania hao,” alisema Mulongo.
Mulongo alisema maofisa wa FBI walifika jana saa tano asubuhi ili kusaidiana na Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika uchunguzi wa tukio hilo. Maofisa hao wa FBI walikuwa Zanzibar ambako walikuwa wanachunguza kifo cha Padri Evaristus Mushi ambaye aliuawa Februari 17, mwaka huu.

Hii itakuwa mara ya pili kwa wageni kuhusishwa na matukio ya ugaidi nchini baada ya mwaka 1998 wakati raia kadhaa wa Misri wakiongozwa Fazul Abdulla waliposhirikiana na Watanzania kadhaa akiwamo Ahmed Ghailani kulipua ubalozi wa Marekani nchini na ule wa Kenya. Ghailani anatumikia kifungo cha maisha nchini Marekani wakati Fazul aliuawa Somalia mwaka 2011.

Tamko la Serikali
Akitoa tamko la Serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alimtaja mmoja wa watuhumiwa wanaoshikiliwa kuhusika na tukio hilo kuwa ni Victor Calisti Ambrose (20), mkazi wa Kwa Mrombo Arusha ambaye ni dereva wa bodaboda. Alisema kijana huyo ndiye anayetuhumiwa kurusha bomu hilo.

Waziri Nchimbi alitoa onyo kali kwa wanasiasa wanaopandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na kuishutumu Serikali kutokana na matukio kama hayo. “Kuna wanasiasa ambao wanaona masilahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania, masilahi yao ni muhimu kuliko utulivu wa Watanzania na masilahi yao ni muhimu kuliko umoja wa Watanzania.”

JK akatiza ziara, Bilal atoa ahadi
Rais Jakaya Kikwete, amekatiza ziara yake ya kiserikali nchini Kuwait ili kurejea nyumbani kutokana na shambulio la bomu kwenye kanisa hilo. Taarifa ya Ikulu imesema jana kwamba Rais Kikwete amelazimika kukatiza ziara hiyo na kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi. Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal ameahidi kuwa Serikali itahakikisha wote waliohusika na tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Balozi wa Papa atoa tamko
Askofu Padilla ambaye jana alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Mkoa, Mount Meru, alieleza kustushwa na tukio hilo na kusema hakutarajia kitu kama hicho kutokea wakati wa shughuli hiyo wakati Watanzania wakijulikana ni watu wa amani. Alilaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.

Kanisa Katoliki Arusha
Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha jana liliitaka Serikali iwataje waliohusika na tukio hilo la kigaidi huku likiwataka waumini wake kutolipiza kisasi.

“Msimamo wa kanisa katika hili, ni kuwataka waumini wasilipize kisasi kama ambavyo alisema Yesu Kristo kuwa msilipize kisasi, muwe tayari kushinda ubaya kwa wema,” alisema Askofu Josephat Lebulu na kuongeza:

Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU)
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (EU), imetaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa tukio hilo na kuonya kuwa matukio kama hayo yanaweza kulitumbukiza taifa kwenye machafuko. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Umoja huo nchini, Filiberto Ceriani-Sebregondi alisema Tanzania inapaswa kufahamu kwamba pasipo kujenga, kuendeleza na kusisitiza utamaduni wa kuvumiliana, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa siku za usoni.

CHANZO: Gazeti Mwananchi