Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Ataka Walevi Kudhibitiwa Rombo

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama

Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas Gama

Yohane Gervas, Rombo

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Rombo kuhakikisha anawaagiza viongozi wote wa vijiji vya wilaya ya Rombo kuweka mikakati na sheria ndogo ndogo kwa kila kijiji za kukabiliana na tabia ambazo hazikubaliki katika jamii ikiwemo vitendo vya ulevi.

Gama aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mokala kilichopo katika tarafa ya Mkuu. Alisema hali hiyo ni kutokana na Wilaya ya Rombo kukithiri kwa vitendo vya ulevi wa pombe.

Alisema kuwa wapo baadhi ya watu ambao wanakunywa pombe kuanzia asubuhi hadi jioni hali inayowafanya kushindwa kufanya kazi na kusababisha migogoro na kuvunjika kwa ndoa nyingi kwani wanapolewa wanasahau na kushindwa kutimiza wajibu wao wa ndoa.

Gama ameongeza kuwa pombe imeharibu sifa ya Wilaya ya Rombo na pia imeharibu mila na tamaduni za wakazi wa wilaya hiyo ambao wengi wao ni wachaga. Alisema kuwa endapo tabia hiyo ya ulevi haitakomeshwa mapema taifa litakosa vijana ambao ndio nguvu kazi.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa wilaya ya Rombo inaongoza kwa kuwa na aina nyingi za pombe za kienyeji kuliko wilaya nyingine zote za Mkoa wa Kilimanjaro ambapo kuna aina zaidi ya hamsini ya pombe za kienyeji jambo ambalo limeharibu sifa na heshima ya wilaya ya Rombo.