Na Janeth Mushi, Thehabari Arusha
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha imetoa magari mawili yenye thamani ya sh. milioni 253.8 kwa Hospitali ya Mkoa huo ya Mt. Meru kwa ajili ya kubebea wagonjwa.
Akikabidhi magari hayo Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isidore Shirima alisema lengo la ofisi yake kutoa magari hayo ni kuiwezesha hospitali hiyo kutoa huduma bora kwa wagonjwa na hata viongozi wa Serikali na Jumiya za Kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirima alisema Mkoa wa Arusha ni Jiji la Kimataifa na kwamba lina taasisi nyingi za kimataifa hivyo huduma za afya zinahitaji kuboreshwa kwa kiwango cha kimataifa na kuutaka uongozi wa hosptali hiyo kuhakikisha magari hayo yanatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.
Akipokea magari hayo kwa niaba ya Hospitali hiyo ya mkoa mganga mkuu wa mkoa Dk. Salash Toure alisema kuwa wanaishukuru serikali kwa kuona umuhimu wa kutoa magari hayo nkwani walikuwa na uhaba mkubwa wa magari ya kubebea wagonjwa.
“Tunashuikuru kupata magari haya na kwamba katika moja ya magari haya gari moja lina vifaa vyote muhimu “resasitation” ambapo mgongwa ataweza kupata huduma zote za matibabu wakati akipelekwa hosptalini akiwa ndani ya gari hilo,” alisema Toure.
Magari hayo yanye namba za usajili STK 8165, thamani ya milioni 142.7 aina ya IVECO litatumika kuhudumia viongozi wa kitaifa na kimataifa (Executive Ambulance) na gari namba STK 8493 Toyota Land Cruiser, thamani ya milioni 111.1 litatumika kubeba wagonjwa wengine wa kawaida.
Wakati huo huo, Shirima aliwataka wakazi wa Mkoa wa Arusha kujitokeza kwa wingi leo katika maaadhimisho ya kusherehekea miaka 50 ya uhuru, ambapo kimkoa yanafanyika Uwanja wa Azimio la Arusha.