Serikali yawataka wakaguzi wa miradi kuwa makini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijjah akifungua mkutano wa siku tatu wa wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa leo jijini Dar es Salaam wenye lengo la kuwaelimisha juu ya marekebisho ya Sheria ya Fedha Sura 348 ya Juni 2010 yaliyopelekea Wizara ya Fedha kuanzisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali (Internal Auditor General Division) ambayo pia inajukumu kusimamia na kuboresha ukaguzi wa ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekrietarieti za Mikoa.

Na Tiganya Vincent, MAELEZO-Dar es Salaam

SERIKALI imewaagiza wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha hesabu za miradi ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi inakaguliwa sawia ikiwa ni pamoja kujiridhisha kuwa inalingana na thamani ya fedha iliyotumika katika matumizi ya mradi husika.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Ramadhan Khijjah alipokuwa akifungua mkutano wa siku tatu kwa wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mkutano huo kwa wakaguzi unalenga kuwaelimisha juu ya marekebisho ya Sheria ya Fedha Sura 348 ya juni 2010 yaliyopelekea Wizara ya Fedha kuanzisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali (Internal Auditor General Division) ambayo pia inajukumu kusimamia na kuboresha ukaguzi wa ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekrietarieti za Mikoa.

Picha ya pamoja ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Ramadhan Khijjah na baadhi ya wakaguzi wa ndani wa Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa baada ya ufunguaji wa mkutano wa siku tatu wenye lengo kuwaelimisha juu ya marekebisho ya Sheria ya Fedha Sura 348 ya juni 2010 yaliyopelekea Wizara ya Fedha kuanzisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani wa Serikali (Internal Auditor General Division) ambayo pia inajukumu kusimamia na kuboresha ukaguzi wa ndani kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekrietarieti za Mikoa ulianza leo jijini Dar es Salaam. Picha zote na Tiganya Vincent, Dar es Salaam.


Khijjah alisema wajibu wa wakaguzi kuanzia Serikali Kuu hadi Serikali za mitaa kuhakikisha kuwa miradi zaidi ya maendeleo inakaguliwa na taarifa kuifikia Wizara ya Fedha mapema ili hatua muafaka ziweze kuchukuliwa kwa lengo la kuboresha dosari zinazojitokeza ili miradi inayopelekwa katika jamii inasaidia e kuleta maendeleo yaliyokusudiwa na wananchi.

“Ni wajibu wenu katika kuongeza uwajibikaji na uwazi katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma, ili Serikali iweze kupata thamani ya fedha zinazotumika na kuboresha huduma kwa jamii,” alisema Khijjah.

Aidha Katibu Mkuu huyo aliwaagiza kuwa wakaguzi hao wa ndani kujielimisha zaidi kwa kusoma miongozo mbalimbali ya ukaguzi wa ndani na namna ya kuweka kumbukumbu vizuri ili kufanya kazi ya ukaguzi katika viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia kuwa watendaji wazuri na wanaotoa taarifa zinazoonyesha ukweli halisi wa matumuzi ya fedha na rasilimali za wananchi kwa ajili ya maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Khijjah alisema kuwa Serikali ilianzisha Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha Sura 348 yaliyopitishwa na Bunge Juni, 2010 kwa lengo ya kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika udhibiti na usimamizi wa matumizi ya rasilimali za umma na Utawala Bora.