Mkutano wa Umoja wa Watanzania Ujerumani na Worldmission Sunday Wafana

Mkutano wa Umoja wa Watanzania Ujerumani na Worldmission Sunday Wafana

*Wahisani washawishika zaidi kusaidia miradi Tanzania!

Watanzania waishio Ujerumani wamejumuika kwa wingi katika Mkutano wa Worldmission Sunday uliofanyika Oktoba 28, 2012. Watanzania hao ambao walitoka pande mbalimbali za ujerumani, walihudhuria mkutano huo ambao ulianza saa nne asubuhi mpaka saa 6 za mchana. Baada ya chakula cha mchana mkutano huo uliendelea hadi saa 12 za jioni. Dk. Isak Majura alitambulisha Taifa la Tanzania kwa kuonyesha Presentation ambayo ilitayarishwa na Jumuiya ya Watanzania Ujerumani (UTU).

Vile vile Katibu wa UTU aliweka mchanganuo wa mradi wa Shule ya Msingi iliyopo maeneo ya Kigamboni Dar es Salaam, ambapo wafadhili kadhaa walionesha utayari wa kutaka kujua ni jinsi gani wanaweza kuifikia shule hiyo ili kuangalia uwezekano wa kuchangia chochote katika maendeleo ya shule.

Mara baada ya kukamilika kwa uwasilishaji wa mradi Mgeni Rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini ujerumani, Bw. Ali Siwa alitoa salam rasmi kutoka Ubalozi wa Tanzania na kuwashukuru watayarishaji wa Mkutano huo kwa upendo wao hadi kuualika Umoja wa Watanzania Ujerumani.

Wakati huo huo Bi. Tabia Mwanjelwa, (Muimbaji wa Maquiz wa Zamani) aliburudisha kwa kuimba na kupiga gitaa, ambapo aliwaacha hoi wafadhili waliohudhuria katika mkutano huo, Bi. Tabia Mwanjelwa alisema sauti yake na utaalamu wake wa kupiga Gitaa ndio mchango wake kwa Watanzania. Watayarishaji wa Mkutano huo wamefurahishwa na wameridhika sana na mahudhurio ya Watanzania, pamoja na presentation zote mbili, na kuahidi kuwa Umoja wa watanzania Ujerumani watapata mialiko mara kwa mara kunapotokea hafla za aina hii.

Umoja ni Nguvu!
kamati.utu@googlemail.com