Mkutano wa Shukrani na Kuombea Tanzania Kitaifa Kufanyika Jumamosi

 

Mratibu wa mkutano wa kitaifa wa kuombea nchi na Rais Dk.John Magufuli, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Abudant Blessing Center (ABC), Askofu Flaston Ndabila (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo ambao utafanyika kesho kutwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Jimbo la Dar es Salaam, Lawrence Kameta  na katikati ni Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maombi ya shukrani kitaifa, Askofu Mkuu wa Naoith Pentekoste Church, Dk. David Mwasota.

 

Na Dotto Mwaibale
 
MRATIBU wa mkutano wa kitaifa wa kuombea nchi na Rais Dk.John Magufuli, ambaye ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Abudant Blessing Center (ABC), Askofu Flaston Ndabila amesema viongozi wa Serikali, kidini na wananchi watakutana kesho kutwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika maombi maalum ya shukrani ya kuiombea nchi pamoja na Rais Dk. John Magufuli ili aweze kuendelea kufanyakazi zake kwa amani.
 
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Askofu Ndabila  maombi hayo yatafanyika Julai 15, mwaka huu katika Uwanja huo na kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchema anatarajiwa kuwa mgeni rasmi. Alisema katika maombi hayo yaliyoandaliwa na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali, I Go Africa For Jesus na wananchi yatatoa fursa ya kuiombea amani nchi.
 
“Hadi sasa kuna wenzetu kutoka nje ya nchi Marekani wameomba kushiriki nasi na tutakuwa pamoja nao wametaka waje wengi lakini imebidi tuweke ukomo,”alisema Mwasota.
 
Alisema lengo kuu la maombi hayo pia ni kumuunga mkono Rais Dk.Magufuli ambaye amekuwa akiomba watanzania wamuombee mara kwa mara.
 
Ndabila  alisema maombi hayo yatatanguliwa na  semina ya siku mbili ya viongozi hao inayo anza leo Kanisa la Assemblies of God kwa Askofu David Mwasota Makuburi External jijini Dar es Salaam. Aliongeza kuwa kataika mkutano huo kila mkoa utawakilishwa na mjumbe mmoja katika maombi hayo.
 
Alisema baada ya maombi hayo kila mkoa utaendelea na maombi yake kulingana na ratiba zao ambapo aliwataja baadhi ya maaskofu watakaohudhuria maombi hayo kuwa ni  ni Dk. Philemon Tibananason, Dk.Bernard Mwaka, Sylvester Gamanywa, Lawrence Kameta, Dk. Barnabas Mtokambali na wengine kutoka nje ya nchi.
 
Alisema waandaaji wa maombi hayo ni Nyumba ya Maombi Tanzania Igo Africa For Jesus na viongozi wa makanisa wa huduma za kikristo Tanzania.
 
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God Jimbo la Dar es Salaam, Lawrence Kameta ambaye anatoka kanisa la  Tabata, alisema shughuli zote za maombi hayo zimepata baraka kutoka uongozi wa juu wa umoja wa  makanisa yaliyoungana kufanya maombi hayo ya kihistoria hapa nchini.
 
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maombi ya shukrani kitaifa, Askofu Mkuu wa Naoith Pentekoste Church, Dk.David Mwasota amesema maandalizi yote ya mkutano huo yamekamilika na kuwa kutakuwa na kwaya mbalimbali zitakazotoa burudani ya nyimbo za kumtukuza mungu ambapo ametumia fursa hiyo kuwaomba wananchi mbalimbali bila kujali dini zao kufika kushiriki maombi hayo ambayo ni muhimu kwa nchi yetu.