CHINA na Urusi zimendelea kushutumiwa vikali kwa kutumia kura ya turufu kupinga azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la kumaliza ghasia nchini Syria, ambako mauaji dhidi ya waandamanaji yanaripotiwa kuendelea.
Mwanaharakati wa vuguvugu la mageuzi katika ulimwengu wa Kiarabu ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya Nobel, Tawakkul Karman, ameulaani vikali utawala wa Bashar al-Assad.
Mtetezi huyo wa mageuzi kutoka Yemen anayehudhuria mkutano wa usalama unaofanyika Munich, Ujerumani, pia alizitaka nchi za Kiarabu kuwafurusha mabalozi wa Syria ili kuonesha ghadhabu yao kuhusiana na ukandamizaji unaoendelea kufanywa na serikali dhidi ya wanaounga mkono demokrasia nchini Syria.
Wito huo uliungwa mkono na Waziri Mkuu wa Tunisia, Hamadi Jebali, ambaye serikali yake ilichukua uamuzi huo hapo awali. Alisema watu wa Syria hawataraji kusikia taarifa ndefu kutoka kwao pamoja na shutuma isipokuwa wanataraji kuona vitendo.
Tunisia, ambako vuguvugu la wimbi la mageuzi lilianzia, imekuwa katika mstari wa mbele kuupinga utawala wa Rais al-Assad. Mazungumzo hayo ya usalama mjini Munich yanafanyika siku moja baada ya taarifa za watu 260 kuuwawa na vikosi vya usalama katika mji wa kati wa Homs kwenye ukandamizaji unaoendelea wa serikali.
-Kwa taarifa zaidi tembelea; http://www.dw.de/dw/0,,11588,00.html