Na Mwandishi Wetu, Tanga
MKUTANO wa Uhamsishaji uliofanyika siku moja tu kabla ya madhimisho ya kilele cha siku ya idadi ya watu duniani jana uliingia dosari baada ya Mwakilishi mkazi wa Shirika la Idadi ya watu na makazi duniani (UNFPA) Christopher Mwaijonga kuanguka na kufariki dunia.
Mwaijonga alianguka wakati wa mapumziko ya chai ikiwa ni muda mfupi tu kabla ya kutakiwa kuwasilisha mada yake katika mkutano huo iliyohusu fursa na changamoto zinazowakabili vijana hapa nchini.
Tafrani ya aina yake ilizuka majira ya saa 6.00 mchana katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga ambapo marehemu akiwa anabadilishana mawazo na wajumbe mbalimbali wa mkutano huo ghafla alianguka na kukoroma mara tatu na kasha kupoteza fahamu.
Kelele za wanawake waliokuwa katika ukumbi huo zilivuma huku wakipiga kelele’jamani hakuna daktari hakuna daktari ndipo walipojitokeza madaktari wawili akiwemo Mganga Mkuu wa halmashauri ya wilaya Korogwe Dk.Rashid Hamza pamoja na Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo Dk.Jumanne Karia.
Kutokana na tafrani hiyo walijitokeza wanaume kadhaa ili kumbeba Mwaijonga(marehemu)na kumuingiza kwenye gari yenye namba za usajili T 256CD35 iliyomkimbiza katika hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo.
Akizungumzia kifo cha marehemu Dk.Karia ambaye alitoka na marehemu tangu kwenye chumba cha mkutano hadi Bombo alisema kuwa Mwaijange alifariki wakati wakiwa njiani wakielekea hospitalini.
Dk.Karia alisema marehemu alipata ugonjwa unaojulikana kama Haemorhegic Strocke ambapo ni mishipa midogo ya damu hupasuka kichwani.
“Inasemekana marehemu alikuwa akisumbuliwa na tatizo la moyo kwani hii ni mara ya pili kwa maelezo tuliyoyapata kuanguka na alifariki wakati tukimkimbiza bombo…alipata Haemorhegic strocke”,alisema Dk. Karia.
Kwa upande wa mwakilishi kutoka Tume ya Mipango, Ofis ya Rais Florance Mwanri alisema NFPA imepoteza mtu mahiri sana na mfanyakazi wa muda mrefu na kwamba walikuwa wakishirikiana kila mwaka kuandaa siku ya idadi ya watu duniani ambayo hufanyika Julai 11 kila mwaka.
“Kweli NFPA imepata pigo kubwa kwani imepoteza kiungo muhimu sana…marehemu tumekuwa tukishirikiana nae kwa hali na mali kila mwaka katika kuandaa siku ya idadi ya watu duniani”, alisema Mwanri.
Naye Mkuu wa mkoa wa Tanga Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo aliyekuwa mwenyekiti wa mkutano huo akifunga kikao hicho alituma salamu za rambi rambi kwa ndugu na jamaa wa marehemu.
“Bwana ametoa na bwana ametwaa jina lake libarikiwe…tuendelee kumwombea mwenzetu kwani njia yetu wote ni moja ..sina la zaidi ila mkutano umefungwa”, alisema Kalembo.
Katika muda wote wa mkutano huo mara tu baada ya kutolewa tangazo la kifo cha Mwaijonga wajumbe wa mkutano huo walionekana kutawalwa na masononeko hali iliyowafanya kushindwa kuchangia jambo lolote kwenye mkutano huo baada ya kuwasilishwa kwa mada husika.
Siku ya Idadi ya watu duniani ambayo huadhimishwa Julai 11 kila mwaka,Kwa mwaka huu itasherehekewa kitaifa mkoani Tanga katika wilaya ya Muheza