Mkurugenzi TCRA akanusha kutapanya fedha

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma

Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoama

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Profesa John Nkoma amepangua hoja kadhaa zilizowasilishwa na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wakati wa vikao vyao.

Katika ufafanuzi wake, Prof. Nkomo alisema fedha zaidi ya sh. bilioni 2.3 ambazo TCRA inadaiwa kutumiwa kwa ajili ya mafunzo ya wafanyakazi watatu pekee na zile bilioni 45 zinazodaiwa kutumika kwenye jengo la makao makuu ya taasisi hiyo yaani Mawasiliano Tower hazikutumika kama ilivyodaiwa na wajumbe wa POAC.

POAC iliibua tuhuma za matumizi mabovu ya TCRA katika vikao vya kamati yake jijini Dar es Salaam vilivyomalizika hivi karibuni. Prof. Nkoma amedai taarifa hizo si zakweli juu ya matumizi mabovu ya fedha kwenye taasisi yake na huenda zinalengo lingine.

Aidha aliseama si kweli kuwa TCRA ilitumia sh. bilioni 2.3 kusomesha wafanyakazi watatu tu bali zilitumika sh. milioni 140 kwa ajili ya mafunzo ya watumishi hao na kiasi kilichosalia kilitumika kufanya mafunzo kwa wafanyakazi wengine 119.

“Hata hicho kiasi cha sh.bilioni 45 kilichodaiwa kuwa tulitumia kujenga jengo letu la Mawasiliano Tower si cha kweli. Taarifa sahihi zipo na zinaonesha jengo limetumia sh. bilioni 35 hadi kukamilika,” alisema Prof. Nkoma.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya bunge pia waliibua tuhuma kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa TCRA ambao kisheria wanatakiwa kuhudhuria vikao mara nne kwa mwaka, wamekuwa wakilipwa posho kila mwezi kwa ajili ya mawasiliano kwa dola za Marekani. Taarifa zinadai Mwenyekiti wa Bodi hulipwa dola za Marekani 350, Makamu dola 300 huku kila mjumbe akipewa dola 250 kwa mwezi. Madai ambayo hata hivyo tayari yamekanushwa na Prof. Nkomo.