Mkurugenzi Takukuru amsafisha tena Chenge!

Mh. Andrew Chenge

* Ni kuhusu suala la rada, adai wezi ni Waingereza

* Asema Chenge anachunguzwa alikopata ‘vijisenti’

Na Mary Mwita, Arusha

MKURUGENZI  wa Taasisisi ya  Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru),  Dk. Edward Hosea amezidi kumsafisha Mbunge wa Bariadi, Andrew Chenge   kuhusu tuhuma za rada.

Amesema Chenge ambaye ni mwanasheria mkuu wa zamani wa serikali,  hausiki na tuhuma hizo ingawa  anachunguzwa kuhusu wapi alikopata ‘vijisenti’ (dola za Marekani milioni moja) zilizokutwa katika akaunti ya kisiwa kimoja cha Uingereza.

Alikuwa akizungumza katika semina ya wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini  katika Hoteli ya Naura Spring mjini Arusha.

Dk. Hosea alisema anashangazwa na waandishi wa habari kushindwa kueleza ukweli kuhusu suala

la rada.

Alisisitiza kuwa uchunguzi umebaini kuwa Waingereza ndiyo wala rushwa na walihusika katika suala  hilo kwa kugawana Dola za Marekani  milioni 40, asilimia 31 zikiwa imetumika

kwenye rushwa ya  kuhalalisha mkataba huo.

Mtu aliyetajwa kwa jina la Vithilan ndiye anadaiwa

kugawa fedha hizo miongoni mwao, alisema.

“Mimi ninawashangaa sana waandishi hawajaeleza umma ukweli kuhusu suala la rada nasema

Chenge … ufafanuzi ulitolewa lakini sikuona mwandishi aliyetoa ufafanuzi.

‘Nasisitiza kesi ya Mbunge huyo ya kujibu ni ya ‘vijisenti’, aeleze alipata fedha hizo wapi, fedha ambazo Mtanzania wa kawaida hawezi kupata,“ alisema Dk.Hosea.

Dk. Hosea alisema pia kuwa ushahidi kuhusu kesi ya Kampuni ya  Kagoda (inayotuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha za EPA), uligonga mwamba baada ya kuonyesha kuwa wadhamini na wakurugenzi wa kampuni hiyo wamekufa na picha zao kukutwa katika jalada.

Hata hivyo, alisema mmoja wa watuhumiwa wa

Kagoda, Mfanyabiashara  Yusuf Maji alirejesha Sh bilioni 40.

Alisema Manji alirejesha fedha hizo  baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kuwa ikiwawatuhumiwa watajisalimisha na kurudisha fedha hizo watasamehewa.

Dk. Hosea alisisitiza kesi hiyo ilikwamishwa na ushahidi wenye utata kwa kubainika kuwa wahusika ni marehemu na ukweli kwmaba  ni  vigumu kumfanyia uchunguzi marehemu .

Mkurugenzi huyo alisema kwa kuwa kesi ya Kampuni ya Kagoda imekuwa ni ajenda kuu ya umma,  Takukuru inajipanga   kufanya uchunguzi tena.

Alisema  mafanikio ya kupata ukweli wa suala hilo yatategemea ushahidi na aliomba watu wenye ushahidi   wajitokeze kuisaidia taasisi hiyo.

“Kwa maslahi ya umma na kutaka umma uridhike na sakata hili, tutarudia uchunguzi kama Takukuru.

‘Tofauti na awali tulivyotumwa na Rais kufuatilia Kagoda,   ninataka niwahakikishie wananchi kuwa Takukuru tunajiendesha wenyewe na hutuendeshwi na Rais kama wengi wanavyodhani na Sheria ya Rushwa inaeleza bayana.

Alimtaka mwandishi wa habari aliyemtaja kwa jina la Mbaraka Ismail (mwandishi wa habari wa gazeti la Kulikoni) aliyedai ana ushahidi wa Kagoda aupeleke ili usaidie ushahidi.

Dk.Hosea aliwataka waandishi wa habari na wahariri kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa

habari za kweli na kueleza umma  pamoja na kuandika habari za maendeleo zenye kubadili hali

za maisha ya watanzania badala ya mabaya kila wakati.

Source: Mtanzania