Mkurugenzi Mpya TAMWA Kukabidhiwa Ofisi Kesho

Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA anayemaliza muda wake, Ananilea Nkya

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimepata Mkurugenzi Mtendaji mpya ambaye anachukua nafasi ya Ananilea Nkya anayemaliza muda wake baada ya kulitumikia shirika hilo kwa miaka 11.

Mkurugenzi huyo mpya wa TAMWA, Valerie Msoka ambaye ni miongoni mwa wanahabari wanawake 12 walioanzisha TAMWA, amefanya kazi za kutukuka katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa. Valerie Msoka atakabidhiwa rasmi ofisi Alhamisi tarehe 27 Septemba katika sherehe fupi itakayofanyika kuanzia saa 3.30 hadi ya 5.00 asubuhi.

Sherehe hiyo itakayofanyika katika ofisi za TAMWA zilizoko eneo la Sinza-Mori, Dar es Salaam inatarajiwa kuhudhuriwa na wahariri na wanahabari kutoka vyombo vya habari mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya wanahabari, Wakurugenzi Watendaji kutoka mashirika ya kiraia na viongozi wa TAMWA wa zamani na sasa.

Valerie Msoka alifanya kazi Radio Tanzania Dar es Salaam, shirika la utangazaji la Uingereza BBC idhaa ya Kiswahili na Kiingereza kabla ya kujiunga na Umoja wa Mataifa. Kadhalika Valerie Msoka mwenye shahada ya Uzamiri katika fani ya Uandishi wa habari wa Kimataifa (M.A in International Journalism) kutoka Chuo Kikuu cha City nchini Uingereza, amefanya kazi kwenye maeneo ya vita ikiwemo Iraq, Sudan, Rwanda, Congo na Burundi.

Valerie Msoka anachukua uongozi wa TAMWA wakati shirika likiwa linajiandaa kuanza kutekeleza mradi mkubwa wenye lengo la kuimarisha vuguvugu katika harakati za kujenga usawa wa kijinsia na kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

TAMWA itatekeleza mradi huo kwa kushirikiana na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Chama Cha Wanasheria Wanawake nchini (TAWLA), Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Kituo cha Usuluhishi (CRC).

Wilaya kumi zitanufaika na mradi huo ambazo ni Wete (Pemba Kaskazini), Unguja Magharibi (Unguja Urban West), Wilaya ya Unguja kusini (Unguja South district), Kisarawe (Pwani), Newala (Mtwara), Mvomero (Morogoro), Lindi vijijini na Ruhangwa (Mtwara), Kinondoni na Ilala, (Dar es Salaam).