Mkurugenzi Mkuu TANESCO, Mhando Atimuliwa Rasmi

William Mhando

Na Mwandishi Wetu

BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imemfukuza kazi Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO nchini, William Mhando baada ya kubainika anamakosa ya kuliingiza mikataba shirika hilo iliyokuwa na mgongano wa maslahi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi leo, Jenerali (mstaafu) Robert Mbona inasema wameamua kumwachisha kazi Mhando baada ya kuthibitika kuwa chini ya uongozi wake amekuwa akikiuka taratibu za shirika na matumizi mabaya ya madaraka.

Katika taarifa ya Mboma alisema baada ya kubaini kuwepo kwa makosa hayo aliitwa na bodi yake ili ajitetee dhidi ya makosa yaliyobainika dhidi yake, lakini licha ya kutoa utetezi wake haukuweza kumsafisha dhidi ya makosa, hivyo kufikia uamuzi wa kumtimua kazi.

Awali Mhando alisimamishwa kazi Julai 16, 2012 na Bodi ya TANESCO baada ya kuwepo na tuhuma dhidi yake, kisha bodi hiyo kumpa kazi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma (CAG), kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizobainika. Taarifa ya CAG ilibaini kuwepo kwa makosa hayo na ndiyo chanzo cha kiongozi huyo kutimuliwa.

“…Aidha, baada ya kupokea taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Mashirika ya Umma, Bodi iliteua Jopo la watu watatu kusikiliza utetezi wa Mhandisi William Geofrey Mhando dhidi ya tuhuma mbalimbali zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Mashirika ya Umma. Baada ya kumsikiliza, Jopo hilo lilikuta Mhandisi William Geofrey Mhando na hatia dhidi ya makosa yanayohusiana na ukiukwaji wa taratibu za shirika, ikiwemo mgongano wa kimaslahi,” alisema Mboma katika taarifa yake ya leo.

Hata hivyo hivi karibuni gazeti moja la kila wiki (Raia Mwema) liliripoti kuwa taarifa ya CAG ilibaini mgongano wa maslahi kwa Mhando. Kwa mujibu wa uchunguzi, Mhando amebainika kuwa na mgongano wa kimaslahi na Kampuni ya MC Donald Live Line Technology Ltd.

Gazeti hilo liliendelea kuwa, kwa mujibu wa nyaraka zilizopo, Mhando ameingia mkataba na MC Donald Live Line Technology Ltd, ikidaiwa alipewa majukumu ya kuitafutia miradi kampuni hiyo ndani ya TANESCO.

Pamoja na kashfa hiyo ya MC Donald Live Line Technology Ltd uchunguzi wa Raia Mwema ulibaini kuwapo pia kwa kashfa nyingine ambayo pia inaonyesha matumizi mabaya ya madaraka, ikiwa nayo inathibitishwa na nyaraka, ikihusu kujipa kazi za shirika analoliongoza hivyo kujiingiza katika mgongano wa kimaslahi. Kashfa hiyo ni ile iliyowahi kuandikwa na gazeti hili iliyohusu kuipa zabuni kampuni iliyohusishwa na mkewe.

Kwa mujibu wa nyaraka ambazo Raia Mwema imeziona kuhusiana na kashfa hizo, Mhando aliingia mkataba na Kampuni ya MC Donald Live Line Technology Ltd akiwa na jukumu la ndani ya kampuni hiyo la utafutaji miradi ikiwamo ile ya TANESCO.

Kutokana na kuwapo kwa taarifa hizo zinazothibitishwa na nyaraka mbalimbali, mwandishi wetu aliwasiliana na Mhando ili kwanza kujua kama anaitambua kampuni ya MC Donald Live Line Technology Ltd na kama anahusika nayo kwa kukabidhiwa jukumu la kuitafutia miradi kampuni hiyo binafsi.