Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es Salaam
VYOMBO vya habari nchini vimeshauriwa kutoa kipaumbele kwa habari zinazojenga jamii kwa kuihamasisha kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo, kudumisha uzalendo na kuepuka habari zinazoweza kusababisha mgawanyiko na chuki katika jamii. Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Msemaji wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Bw. Assah Mwambene alipotembelea ofisi ya gazeti la Jamhuri iliyopo Mtaa wa Samora jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa idara hiyo kuvitembelea vyombo anuai vya habari kwa lengo la kudumisha ushirikiano na kujadili changamoto mbalimbali za tasnia ya habari nchini.
Alisema Serikali inaheshimu mchango mkubwa unaotolewa na tasnia ya habari hapa nchini na kuongeza kuwa habari ni moja ya sekta inayokuwa kwa kasi, yenye uwekezaji mkubwa na inayoajiri watu wengi hapa nchini. “Sisi kama Serikali ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tasnia ya habari hapa nchini inapiga hatua kutokana na umuhimu wa pekee ilio nao katika jamii, hivyo utaratibu huu wa kuvitembelea vyombo vya habari ni wa kawaida ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujadili namna ya kutatua changamoto mbalimbali zilizopo,” alisema Mwambene.
Akizungumza na wahariri wa gazeti hilo, Mwambene alisema kuwa vyombo vya habari hapa nchini vina wajibu mkubwa wa kuhakikisha vinatoa kipaumbele kwa habari zinazogusa masuala mbalimbali ya wananchi na kuibua changamoto mbalimbali zilizo katika jamii kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ustawi wa taifa. Aidha alilipongeza gazeti hilo kwa kuendelea kuzingatia weledi katika utoaji wa habari zake kwa kuweka msisitizo wa utoaji wa habari zinazohamasisha uzalendo.
“Kwanza nawapongeza kwa kazi mnayoendelea kuifanya hasa moyo wa uzalendo mliouonesha mlipokuwa mkiandika habari na kuchapisha makala kuhusu uhusiano wa Tanzania na nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia katika masuala mbalimbali yenye kuhamasisha uzalendo nchini,” alisema Mwambene.
Ameeleza kuwa hivi sasa taifa la Tanzania liko katika mchakato wa masuala makubwa yanayogusa maisha ya watu na maendeleo yao yakiwemo ya Uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao na zoezi linaloendelea la kupata katiba mpya na kufafanua kuwa katika hilo vyombo vya habari vina wajibu wa kuhamasisha umoja wa kitaifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari – Usajili wa Magazeti, Raphael Hokororo alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa taaluma ya habari inaendelea kulindwa hapa nchini na waandishi wa habari wanafanya kazi zao bila vikwazo, idara ya Habari imekuwa ikitoa vitambulisho vya waandishi wa habari (Press Card) kwa waandishi wenye sifa na taaluma ya habari. Alisema utoaji wa vitambulisho kwa waandishi wa habari umesaidia kudhibiti uwepo wa waandishi wasio na sifa katika shughuli mbalimbali za serikali ikiwemo mkutano wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea mjini Dodoma.
“Katika hili tumeweka msisitizo wa matumizi ya vitambulisho hivi na tumeanza na Bunge maalum la Katiba waandishi wote wanaoandika habari za bunge la katiba tumewapatia vitambulisho.” Alisema Hokororo.
Akizungumza Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile aliwapongeza viongozi wa Idara ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara hiyo, Mwambene kufuatia utaratibu huo wa kuvitembelea vyombo vya habari na kuongeza kuwa unaongeza ushirikiano baina ya vyombo vya habari na serikali.
Akizungumzia juu ya mchakato wa kupata katiba mpya na uchaguzi mkuu ujao, Balile ameeleza kuwa gazeti la Jamhuri linaendelea kutoa kipaumbele kwa habari zenye maslahi kwa taifa na pia habari za vyama vya siasa vyenye kujenga hoja kwa wananchi.
Aidha amesema kuwa wao kama chombo cha habari makini wataendelea kuihabarisha jamii kwa kuzingatia maadili, uzalendo na kukemea vitendo viovu vinavyorudisha nyuma maendeleo ya taifa.