Mkuranga na Ukombozi Kiuchumi Toka MKURABITA

Mmoja wa wanakijiji wa Mwarusembe wilayani Mkuranga akipokea hatimiliki ya ardhi ya kimila toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Silla katika hafla hiyo ya hivi karibuni.

Mmoja wa wanakijiji wa Mwarusembe wilayani Mkuranga akipokea hatimiliki ya ardhi ya kimila toka kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Silla katika hafla hiyo ya hivi karibuni.


*‘Hatimiliki za ardhi ni pasipoti kuelekea uchumi rasmi’        
*Benki zatakiwa kuzitambua kwa mikopo
 
“Tumieni hati kutafuta mikopo yenye thamani kubwa ili iwaletee maendeleo sio kutumia hati yenye thamani kubwa kama hii, kupata mkopo wa kufuga kuku kumi. Kama ni ufugaji, fanyeni ufugaji wa kisasa wenye tija.”
 
Anaasa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mercy Silla katika hotuba yake kabla ya kukabidhi rasmi hatimiliki za ardhi za kimila 227 kwa wananchi na wakulima wa Kijiji cha mwarusembe kilichopo wilayani kwake. Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni kijijini hapo. Akaongeza, “Ukiwa na hati hii, umewezeshwa kuingia katika hatua nyingine ya maisha hivyo, lazima mjivunie.”
 
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lunyela, Said Abdalla Mpwepwe aliyepata hati tatu za mashamba tofauti amesema, mpango mkubwa alio nao katika eneo lake ni kilimo chenye tija.
“…Tunahitaji elimu zaidi ili tunufaike  hasa na miradi itakayotupa tija zaidi.’
 
“Kubwa zaidi, nashukuru wadau wote wa urasimishaji huu na MKURABITA kwa namna ya kipekee kwani wamewezesha mashamba yangu sasa yawe dhamana ya kisheria na sasa ni maeneo rasmi yasiyo na migogoro ya mipaka,” amesema Mpwepwe.
 
Naye Hadija Hassan Maninja mwenye hati 1MKR/45 amesema anaamini hati hiyo itamsaidia kuweka mambo yake sawa. Akasema, hataruhusu hati hiyo iwe pambo kabatini, wakati ina uwezo wa kumuinua kiuchumi. Akaongeza, “Mume wangu (Salumu Hemed Jommo) na yeye amepokea ya kwake… Nitangalia cha kufanya, lakini  Mungu atawajalia sana hawa MKURABITA.”
 
Hawa Amiri Kambangwa akasema, “Kwa sasa naweza kukopeshwa na benki na sasa nitabuni mradi utakaoleta faida kwenye familia yangu. Nawashukuru MKURABITA maana wamefanya mashamba yangu kuwa bora na hata mwenyewe sasa nitakuwa bora.”
 
Kwa upande wake, Juma Said Njechele, amesema MKURABITA ni mkombozi wa Watanzania wanyonge na kwamba yeye amekombolewa kwa sasa hata  benki zitamthamini na kumkopesha. “Sasa nahitaji elimu zaidi ili ninufaike zaidi,” amesema Njechele.
 
Katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mwarusembe wilayani Mkuranga katika Mkoa wa Pwani Omari A. Mfilisi, alisema katika hafla kuwa hati hizo zitawafanya waliozipata kunufaiska zaidi na mashamba na ardhi zao kwa kuwa zimeongezeka thamani.
Gloria akikabidhi salamu za MKURABITA kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Silla.

Gloria akikabidhi salamu za MKURABITA kwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Bi. Mercy Silla.


Akasema, “Mradi tuliupokea Novemba 2010; kisha tukapewa wataalamu waliotoa elimu kwa kamati mbalimbali za utekelezaji wa mradi ikiwa ni pamoja na kuzijengea uwezo kwa muda wote wa uandaaji na utekelezaji mradi huu.”
 
Anasema, “Kupitia mikutano ya hadhara, wananchi hao waelimishwa juu ya kusudio la mradi pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi bora ya ardhi.”
 
Mfilisi amefahamisha mbele ya Mkuu wa Wialaya kuwa, kupitia mikutano ya kijiji wananchi hao walibainisha kuwapo kwa maeneo ya mashamba, mashamba na makazi, vyanzo vya maji, misitu na eneo la malisho na  maeneo ya shughuli za huduma za kijamii kama elimu, afya, michezo na makaburi.
 
“Baada ya upimaji, eneo letu limebainika kuwa na ukubwa wa hekta 3,734. Mashamba yaliyopimwa ni 1200 na hati zilizokwishaandaaliwa ni 727.”
 
Anaongeza, “Idadi hiyo imepungua kutokana na baadhi ya wakulima kutoonekana picha zao kama ilivyokusudiwa…”
 
Hata hivyo akasema wazi, “Baadhi ya wananchi wamevamia chanzo cha maji cha Ziwa Manze na kuharibu kabisa uoto wa asili oka eneo hilo.”
 
Kwa niaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Raslimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) wilayani Mkuranga, Sylvester Marwa anasema, “Mpango huu ulijihushsa na vijiji viwili ya Mwarusembe na Mkiu.
 
Anasema, “MKURABITA walivijengea uwezo na hatimaye, kuvisaidia vijiji hivi katika kutayarisha mpango wa matumizi ya ardhi,” anasema Marwa.
 
Anafafanua, “MKURABITA kwa kushirikiana na Income Generating Activities (IGA) walianza kutekekeza machakato wa kuwapatia hatimiliki za kimila za ardhi za wananchi wa vijiji hivyo.”
Wananchi wa kijiji cha Mwarusembe wilayani Mkuranga wakisubiri kwa hamu kukabidhiwa hatimiliki za ardhi za kimila katika hafla iliyofanyika hivi karibuni kijiji hapo. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi. mercy Silla (Hayupo pichani).

Wananchi wa kijiji cha Mwarusembe wilayani Mkuranga wakisubiri kwa hamu kukabidhiwa hatimiliki za ardhi za kimila katika hafla iliyofanyika hivi karibuni kijiji hapo. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga Bi. mercy Silla (Hayupo pichani).


Marwa ambaye ni Mpima Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga anafahamisha, “Mashamba 2000 yalitambuliwa katika vijiji hivi viwili kwa kutumia GPS; mashamba 1200 katika Kijiji cha Mwarusembe na Mashamba 800 katika kijiji cha Mkiu.”
 
Baada ya kutambuliwa, mashamba 1804 yaliandaliwa hati wakati 196 hayakuandaliwa hati kutokana na sababu mbalimbali kama vile kutoonekana vizuri kwenye GPS.”
 
Hata hivyo Marwa anasema, “Jitihada zinaendelea kufanyika ili alama zote ziweze kuonekana na ili kuandaliwa hati.”
Anasema changamoto nyingine iliyolikumba zoezi hilo na kuchelewesha kukamilika kwake ni pamoja na kukosa majirani na picha.”
“Taratibu za kupata picha na majirani zinaendelea kufanyika kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji na wananchi wenyewe,” amefahamisha.
Marwa anatoa tumaini jipya kwa wananchi wa Mkuranga akitamka mbele ya umati, “Leo tunagawa hati 227 ambazo zimekamilika na ziko tayari kwa matumizi. Hati nyingine 992 zimesainiwa na wenye hati, zimesajiliwa vijijini, lakini hazijasajiliwa wilayani kutokana na sababu mbalimali.”
 
Marwa anafahamisha kuwa, licha ya changamoto walizokumbana nazo ukiwamo uhaba wa fedha, ukosefu wa masjala ya ardhi ya kijiji na ukosefu wa afisa ardhi mteule, wamefanikiwa kupata kiasi kadhaa cha pesa toka kwa wadau mbalimbali.
 
Anasema, “Zoezi hili lililpangwa kutumia shilingi milioni 338 za Kitanzania kwa vijiji sita ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi, kujenga masjala za vijiji, lakini ni jumla ya shilingi milioni 71 pekee zilizotolewa na kutumika.”
 
Anasema kazi hiyo imegharimiwa na wadau kadhaa ambapo MKURABITA wamechangia shilingi milioni 21, IGA wamechangia shilingi milioni 46 na Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga imechangia shilingi milioni 4.
 
“Tunawashukuru sana MKURABITA na IGA kwa kuwezesha kusaidia kutoa fedha, utaalamu na vifaa ambavyo kwa pamoja, vimefanikisha ugawaji wa hati miliki za kimila. Tunawaomba wasichoke kuchangia kuendeleza juhudi hizi katika vijiji vingine,” amesisitiza Marwa.

Akizungumza kwa niaba ya Mratibu wa MKURABITA, Seraphia Mgembe, Gloria Mbilimonywa amesema, “Utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo ya maboresho ya urasimishaji ardhi vijijini unawagusa watu wengi zikiwamo asasi za kiraia, wadau wa maendeleo, sekta binafsi na sisi wenyewe ambao ndio walengwa wakuu.”
 
Kwa kutambua hilo, kazi hii ilifanywa kwa ushirikiano wa utatu baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, BTC na MKURABITA. Tunawashukuru sana BTC kwani wao ndio waliofikiria kutekeleza zoezi waliloliita, “Shughuli za kuzalisha Kipato.”
 
Akasema, “…Kumekuwapo changamoto kadhaa katika utekelezaji, lakini kubwa zaidi ni ile ya ukosefu wa afisa ardhi mteule ambaye uwepo wake ni muhimu katika kuhakikisha hati hizi zinapatikana kwa wakati na kutumika kwa wakati…”
 
“Ninauomba uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kulivalia njuga suala hili na kuhakikisha inapata afisa ardhi mteule wake.”
 
Akawataka wananchi waliokabidhiwa hatimiliki hizo za kimila wazitumie kikamilifu kadiri fursa zinavyopatikana ili kujiletea manufaa zaidi kiuchumi kama ilivyo dhana ya MKURABITA.
 
“Uwezeshaji wananchi kutumia rasilimali na biashara zao kama chanzo cha kujiongezea mitaji ni nyenzo ya kupanua wigo wa ushiriki katika shughuli za uchumi wa kisasa.”
 
Akasisitiza, “Nia thabithi ya MKURABITA ni kurudi baadaye katika maeneo ambayo urasimsihaji umefanyika ili kutoa mafunzo kwa wananchi namna ya kuona fursa  na kuzitumia fursa zilizopo katika kukuza mitaji kwa sababu jitihada za makusudi zinahitajika kuzifanya hati hizi ziwe na maana zaidi kwenu na zisiwe mapambo tu.”
 
 “Katika upatikanaji wa mitaji, urasimishaji ni nyenzio na daraja muhimu katika ukuzaji wa miradi… hatimiliki hizi ni sawa na pasipoti katika safari ya kwenda kwenye uchumi rasmi unaotawaliwa na sheria,” akasisitiza
 
“Hivyo, kupitia hati hizi, tufungue macho yetu zaidi katika kuangalia na kutafuta fursa zaidi za kiuchumi zinazoweza kupatikana ili raslimali zetu hizo, zitumike kwa manufaa zaidi katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi.”
 
Kwa upande wa taasisi za fedha yakiwamo mabenki, MKURABITA inatoa wito maalumu.
 
“Wenzetu wa taasisi za fedha, tunawaomba mzitambue na kuzikubali hati hizi kwa kuzipokea na kuzitumia mkizitambua kama dhamana kwa ajili ya maombi ya wananchi wanaohitaji mikopo ili kukuza mitahji yao na kuboresha shughuli zao za kiuchumi.”
 
“Inapobidi basi, mtoe hata mafunzo kwa walengwa hata kama MKURABITA haijakamilisha kupanga kujipanga kwa saabu naamini kwenu vyombo vya fedha, hii ni biashara tena biashara nzuri.”
 
Mbilimonywa kwa niaba ya Mratibu wa MKURABITA amesisitiza kuwa, maboresho ya kisheria na kitaasisi yaliyoandaliwa na MKURABITA ni hai na ENDELEVU.
“Tulichojifunza hapa Mkuranga kitatusaidia kuimarisha mapendekezo yetu juu ya mabadiliko mbalimbali ya sheria ya ardhi yaliyomo kwenye maboresho tunayotekeleza.”
 
CHANZO: DIRA YA MTANZANIA (Joseph Sabinus)