Na Lydia Churi-MAELEZO, DODOMA
SERIKALI imesema kupitisha mkongo wa taifa wa mawasiliano chini ya nyumba hakuna madhara yoyote kwa afya ya wananchi wanaoishi kwenye nyumba hizo wala kwa nyumba zenyewe.
Akijibu swali Bungeni mjini Dodoma leo, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Charles Kitwanga alisema Mkongo wa Taifa hauna madhara yoyote ya kiafya mahali unapopita kwa kuwa hupitishwa chini ya nyumba mita tatu kwenda chini.
Akifafanua, Mheshimiwa Kitwanga alisema wakati wa ujenzi wa mkongo huo, imebainika kuwa baadhi ya wananchi wamejenga nyumba ndani ya hifadhi ya barabara, hivyo ili kuendana na sheria ya hifadhi ya barabara, wizara imelazimika kupitisha mkongo chini ya nyumba hizo.
Aliongeza kuwa serikali inaangalia namna ya kulipa fidia kwa nyumba zilizobomoka baada ya kupitisha mkongo huo na fidia hiyo itatolewa kwa nyumba zilizokuwa zaidi ya mita 22 kama sheria ya zamani ya hifadhi ya barabara inavyosema. Kwa mujibu wa mabadiliko ya sheria ya hifadhi ya barabara, hifadhi ya barabara ni mita 30 kutoka katikati ya barabara.
Naibu waziri huyo alisema mkongo wa taifa wa mawasiliano hujengwa ndani ya hifadhi ya barabara, reli na nguzo za umeme za Tanesco ambapo wizara imekuwa ikiomba vibali kwa taasisi husika ili kutumia hifadhi hizo katika ujenzi wa mkongo huo.
Alisema sehemu kubwa ya mkongo wa taifa wa mawasiliano umewekwa kwenye hifadhi ya barabara zinazomilikiwa na TANROADS ambao wametoa kibali cha kujenga mkongo huo ndani ya mita moja ya mwisho ya hifadhi ya barabara yaani kati ya mita 29 na 30.
Mheshimiwa Kitwanga alikuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Kibiti Mheshimiwa Abdul Jabir Marombwa aliyetaka kujua ni kwa sababu gani mkongo wa taifa upitishwe chini ya nyumba za watu na ni madhara gani yanaweza kuwapata watu wanaoishi kwenye nyumba hizo.