Na Shomari Binda wa Binda News Musoma
UKATILI uliofanywa na madaktari nchini Tanzania unaonesha kuwa Mkoa wa Mara ndio unaoongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa asilimia 72 ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma wenye asilimia 71.
Utafiti huo uliohusu ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto ulifanyika mwaka 2010 na kuonesha kuwa Mkoa wa Tanga ndio wenye kiwango kidogo kabisa cha ukatili nchini.
Takwimu hizo zimeelezwa mjini Musoma na daktari bingwa wa magonjwa ya watoto kutoka kitengo cha afya ya uzazi na mtoto cha Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Grace Mallya wakati wa mkutano wa uhamasishaji viongozi wa mkoa na wilaya kuhusu mwongozo wa kisera na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia na ukatili wa watoto.
Akifungua mkutano huo mkuu wa mkoa wa Mara John Tuppa amesema vitendo vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vikiwemo vya kuwanyanyasa watoto kimwili na kingono kwa kuwalazimisha kufanya vitendo vya ngono bila ridhaa yao, usafirishaji wa wanawake na watoto kwa ajili ya kufanya biashara ya ngono na kuwanyima haki ya kurithi mali za familia bado ni changamoto kubwa katika jamii.
Amesema Serikali imetengeneza mwongozo wa kisera na mwongozo wa kutoa huduma kwa waathrika wa ukatili wa kijinsia ikiwemo ukatili dhidi ya watoto na kusema kuwa miongozo hiyo inatoa maelekezo pamoja na taratibu za kufuata katika kutoa huduma kwa watu walioathrika na ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kwamba suala la ukatili wa kijnsia na ukatili dhidi ya watoto ni suala mtambuka ambalo linagusa sekta mbalimbali na kwa hali hiyo amewashauri viongozi katika ngazi zote kuimarisha ushirikiano kati ya sekta zote zinazohusika na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na watoto ili kuhakikisha kuwa waathirika wanapata haki zao za kisheria na huduma.
Amedai jamii nzima inapaswa kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia vinakomeshwa hususani katika Mkoa wa Mara na kuacha kuiachia kazi hiyo Serikali na Taasisi nyingine zinazojishughulisha na masuala ya kuzuia unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.
Awali kaimu mratibu wa jinsia kitengo cha afya ya uzazi na mtoto kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Martha Rimoy amesema Tanzania ni moja kati ya nchi 14 zilizofanya utafiti wa masuala ya ukatili katika Afrika na kubaini kuwa ina asilimia 44 ya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.