Na Dotto Mwaibale
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya (CCM), ambaye ni diwani wa Kata ya Kiwira, John Mwankenja, ameuawa kwa kupigwa risasi tatu kichwani na watu wasiojulikana.
Tukio hilo ambalo limewasikitisha watu wengi waliokuwa wakimfahamu marehemu limetokea juzi saa tatu usiku muda mfupi baada ya kuwasili nyumbani kwake akitokea mkoani Mbeya kumuona mkewe Lyidia Mwakatumbula ambaye amelazwa hospitali ya wazazi ya Meta kwa matibabu.
Akizungumza kwa njia ya simu na Jambo Leo mdogo wa marehemu Alinanuswe Mwankenja alisema kifo cha kaka yake kimewashitua na kuwatia simanzi kubwa.
“Kaka alikuwa ni tegemeo kubwa katika familia yetu mpaka sasa tunashindwa kujua hawa wauaji walikuwa na nia gani naye” alisema Mwankenja.
Alisema akiwa safarini kutoka Mbeya mjini kurudi nyumbani kwake kwenye mji mdogo wa Kiwira ambako amejenga jirani na mareheme, kaka yake mkubwa Banabas Mwankenja anayeishi Dar es Salaam alimpigia simu kumjulisha juu ya tukio la kifo hilo lakini hawakuelewana.
“Kaka Banabas alinipigia kunijulisha juu kifo hicho kwa kuwa nilikuwa ndani ya basi hatukuelewana lakini wakati huo huo mke wangu alinijulisha kuwa kaka yangu ameuawa na maiti yake bado ipo kwenye gari” alisema
Alisema baada ya kufika nyumbani alijulishwa na mtoto wa marehemu Weston Mwankenja ambaye anasoma kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Ndembela kuwa alipotoka kumfungulia mlango baba yake kabla hajashuka kwenye gari lake walitokea watu watatu wenye silaha.
Aliongeza kuwa watu hao ambao walivalia kininja na kuficha sura zao walimuamuru ashuke kwenye gari na kabla hajafanya chochote walimminia risasi tatu mfufulizo kichwani na kufumua ubungo wake na kufariki papo hapo kumuacha akiwa katika gari lake ambalo lilikuwa halijazimwa.
Katibu Mwenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mbeya Bashiru Madodi, alisema bado hawajajua chanzo cha mauaji hayo.
“Ni mapema kuzungumzia kifo hicho kwani bado tupo hapa hospitali ya Makandana ulipohifadhiwa mwili wa marehemu tutatoa taarifa baadaye kwa sasa tunawaachia polisi waendelee na uchunguzi wao.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Mpandapanda alichokuwa akiiishi marehemu, Michael Kyotamawe, amedai kuwa mauaji hayo yanahusishwa na masuala ya kisiasa kutoka kwa watu waliokuwa wakiwania nafasi ya uongozi wa udiwani wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika oktoba mwaka jana.
“Ni masuala ya kisiasa ndiyo inaweza kuwa chanzo cha kifo cha ndugu yetu kwani hakuwa na ugomvi na mtu isitoshe hao wauaji kama walikuwa ni majambazi wa kutaka kuiba wangeiba lakini wao wamefanya mauaji na kukimbia” alisema Kyotamawe.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Dk.Sungwa Ndagabwene alilithibitia Jambo Leo kutokea kwa kifo hicho alipozungumza jana kwa njia ya simu.
“Ni kweli mwenyekiti wetu wa Halmashauri John Mwankenja, amefariki na mwili wake ulipokelewa hospitali ya Makandana saa 5 usiku juzi ukiwa na majeraha makubwa kichwani na sasa tupo na ndugu, jamaa zake pamoja na polisi tunasubiri kuufanyia uchunguzi mwili wake” alisema Dk.Ndagabwene.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ACP Advocate Nyombi hakuweza kupatikana ili kuzungumzia suala hilo baada ya simu zake zote kutopatikana.