Askari waliogombea mirungi wasubiri hukumu

Inspekta Generali wa Polisi Tanzania, Said Mwema akisalimia Makamanda wake.

 

 

 

Na Mwandishi Wetu,
Mwanza

ASKARI polisi wawili wanaodaiwa kupigana baada ya kushindwa kugawana dawa za kulevya aina ya mirungi iliyotelekezwa na abiria mmoja hivi karibuni mjini hapa wameshitakiwa kijeshi na Jeshi la Polisi na sasa wanasubiri kuhukumiwa.

Akizungumza na Jmwandishi jana mjini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza, Simon Sirro amesema askari hao tayari wameshtakiwa kijeshi na sasa wanasubiri kusomewa hukumu juu ya kosa lao.

Alisema askari hao anasubiri maamuzi kwa ajili ya kuchukua hatua zinazostahili dhidi yao, japokuwa hakufafanua ni hatua zipi watachukuliwa askari hao baada ya kitendo chao cha kulidhalilisha Jeshi la Polisi.

Askari hao walipigana na kujeruhiana Mwezi Machi majira ya saa saba na nusu, mwaka huu katika kituo cha mabasi cha Buzuruga. Tukio hilo liliwahusisha askari polisi wenye namba G 2748 (PC Daniel) wa kituo cha Nyakato na G 3704 (PC Willy) wa kituo cha Mjini Kati.

Watu walioshuhudia ugomvi huo walidai chanzo cha askari hao kupigana walikuwa wakigombea begi la dawa za kulevya aina ya mirungi lililotupwa na mmoja wa abiria wa basi la Zuberi toka Musoma akikwepa kukamatwa askari hao.

Begi hilo leusi lilikuwa la abiria mmoja mwanamke ambaye alishuka nalo kwenye gari kabla ya kulitupa akihofia kukamatwa na PC Daniel na baadaye kutokea PC Willy kasha wote kuanza kumnyang’anya mwenzake akitaka wagawane.

Askari hao ambao walikuwa katika mavazi ya kiraia, walijikuta wakizipiga na kuumizana kabla ya kutiwa mbaroni na askari wa doria na kupelekwa katika kituo cha mjini kati ambako waliswekwa mahabusu.

wakati askari hao wakipigana kulikuwa na wenzao wengine watatu wakivizia kumkamata abiaria huyo. Hata hivyo Jeshi la Polisi hivi karibuni limekuwa katika kashfa ya kuibiwa ama kupotea kwa vielelezo vya dawa za kulevya kutoka kwa watuhumiwa mbalimbali.

Aidha mkoani Mwanza askari kadhaa wanadaiwa kujihusisha na mtandao wa kulinda wafanyabishara wa mihadarati aina ya mirungi na wakati mwingine kuwalinda wafanyabiashara kupita katika vizuizi vya polisi wanapopeleka shehena hiyo sokoni.

Ofisa mmoja wa jeshi akizungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutotajwa jina alikiri kuwa baadhi ya askari wanafanya kazi hiyo na kudai hata pale wafanyabiashara hao wanapokamatwa na kufikishwa mahakamani huachiwa huru kutokana na udhaifu wa ushaidi kisheria.