Mama Salma Awataka Wanafunzi Kutochanganya Mapenzi na Shule

Mama Salma Kikwete mke wa Rais wa Tanzania

Na Anna Nkinda – Maelezo

MKE wa Rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete amewataka wanafunzi wa kike nchini kutochanganya mapenzi na shule kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kupata maambukizo ya virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi pamoja na ujauzito.

Mama Kikwete ambaye pia ni mlezi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mandera iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani aliyasema hayo jana wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kuwatakia heri wanafunzi wa kidato cha nne wanaotarajia kuanza mitihani yao ya mwisho mapema mwezi ujao.

Aliwataka wanafunzi kutumia muda wao wa masomo kwa manufaa ikiwa ni pamoja na kusoma kwa bidii ili kuweza kutimiza ndoto zao katika maisha, jambo ambalo litakuwa pia na manufaa kwa taifa kwa kuwa na wataalamu wengi wa fani mbalimbali.

“Jiepusheni na mazingira yatakayowapelekea kupata ujauzito na kukatisha masomo yenu kwani mimba ni adui wa maendeleoa ya msichana, inatia uchungu kuona mwanafunzi anapata ujauzito lazima mjitambue kuwa ninyi ni wa thamani mnatakiwa kujitunza,” alisema Mama Kikwete.

Kuhusiana na maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi Mama Kikwete alisema kuwa hivi sasa watu wengi wamekuwa na tabia ya kuwa na mpenzi zaidi ya mmoja na kama mmoja wao atakuwa amepata maambukizi ni rahisi kuwaambukiza wote aliopo katika mtandao huo wa mapenzi.

Mlezi huyo wa shule aliwaasa wanafunzi hao kuridhika na vitu wanavyopewa na wazazi wao hata kama ni vidogo lakini kama hawataridhika na kutaka kupata vitu vingi vyenye thamani kwa njia ya mkato matokeo yake ni kupata ujauzito na ugonjwa wa Ukimwi. .

Akisoma taarifa ya shule hiyo Mkuu wa Shule Rose Umila alisema kuwa mahudhurio ya baadhi ya wanafunzi yamekuwa siyo mazuri kutokana na baadhi ya wazazi kuwa na uelewa mdogo juu ya kuwaelimisha watoto wa kike na baadhi yao kutowasomesha watoto wa kike kwa madai ya kipato duni hali inadhorotesha maendeleo ya mtoto wa kike.

Umila alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa vitano, maabara tatu, maktaba moja, mabweni manne, bwalo moja na matundu ya vyoo ishirini, mabafu 12, stoo moja, nyumba za walimu 20 na jengo la utawala moja.

Kwa upande wa thamani shule hiyo inaupungufu wa meza 361, viti 259, meza za walimu tano, na viti vya walimu vitano hata hivyo kwa kushirikiana na wazazi shule hiyo imeweza kutengeneza meza na madawati 50, meza saba na maabara.

Shule ya Sekondari ya wasichana Mandera ambayo kwa mwaka huu itatoa wanafunzi wa kidato cha nne kwa mara ya kwanza inawanafunzi 590 ambao kidato cha kwanza ni 120, cha pili 121, cha tatu 181 na cha nne 178 na walimu 12 kati yao wa masomo ya sanaa tisa na sayansi watatu.