Mke wa Rais wa China Ahaidi Kuisaidia Sekondari ya WAMA

Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan (kulia) akizungumza na mke wa rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete.

Mke wa Rais wa China Mama Peng Liyuan (kulia) akizungumza na mke wa rais wa Tanzania, Mama Salma Kikwete.

Na Anna Nkinda – Beijing, China

MKE wa Rais wa China Mama Peng Liyuan ameahidi kutoa vifaa vya shule vikiwemo vya maabara pamoja na vitabu kwa ajili ya shule ya Sekondari ya WAMA – Nakayama ili wanafunzi hao waweze kusoma vizuri masomo ya sayansi. Mama Liyuan aliitoa ahadi hiyo jana wakati akiongea na mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika ukumbi maarufu wa watu (Great hall of the People) uliopo mjini Beijing.

“Nina mapenzi na Taasisi ya WAMA, nakupongeza kwa kazi unayoifanya ukiwa Mke wa Rais ya kuwainua wanawake kiuchumi na kuwasaidia watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi ambao nao wanapata elimu sawa na watoto wengine.”

Najua kitaaluma wewe ni mwalimu na unapenda shule mwaka huu nitakuunga mkono zaidi katika masuala ya shule, hii itawasaidia wanafunzi kusoma vizuri. Pia nitakuwa na ushirikiano endelevu na Taasisi ya WAMA,” alisema Mama Liyuan.

Kwa upande wake Mama Kikwete alishukuru kwa msaada huo na kusema kila kwenye maendeleo changamoto hazikosekani alizitaja changamoto zinazoikabili sekta ya elimu ambazo ni upungufu wa maabara, kutokuwepo kwa wataalamu wa maabara na walimu wa masomo ya sayansi wa kutosha.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema  katika upande wa elimu Serikali kwa kushirikiana na wananchi wamejitahidi kujenga shule nyingi za Sekondari lakini  bado kuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, kutokuwa na maabara za kutosha, kutokuwa na vifaa vya maabara na  upungufu wa wataalamu wa maabara .

“Ninaomba kuwe na ubadilishanaji wa ujuzi wa kazi (Exchange Program) kwa walimu wetu wa nchi hizi mbili hii itawasaidia kupata utaalamu zaidi katika fani zao na kutoa mfano wa wataalamu wa maabara ambao wakija nchini watasaidia kwa kiasi kikubwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa njia ya vitendo,” alisema Mama Kikwete.

Shule hiyo ambayo inamilikiwa na Taasisi ya WAMA wanafunzi wake ni watoto wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika mazingira hatarishi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani iko kijiji cha Nyamisati wilaya ya Rufiji mkoani Pwani. Hii ni mara ya pili kwa Mama Liyuan kuiunga mkono Taasisi ya WAMA ambapo mwaka 2013 alipotembelea nchini alitoa Yuan milioni moja sawasawa na shilingi milioni 250 za kitanzania na mabegi ya shule 100 kwa ajili ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama na vyerehani 20 kwa ajili ya Umoja wa Vikundi vya WAMA (UVIMA).

Mama Kikwete ameambatana na mumewe Rais Prof. Jakaya Mrisho Kikwete nchini China kwa ziara ya kikazi ya siku sita.