Thehabari.com, Moshi
MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Happyness Mrema (28) amemchoma kisu mumewe
Audiphas Mrema (30) na kumuuwa kutokana na ugomvi wa wivu wa mapenzi. Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro Robert Boaz, alisema tukio hilo lilitokea Machi 9, 2013 katika Kijiji cha Kikelelwa wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, ambapo mwanamke huyo alimchoma kisu mumewe na kumsababishia mauti papohapo.
Kwa mujibu wa Kamanda Boaz, siku ya tukio marehemu alifika nyumbani saa moja usiku na kumkuta mkewe amenuna ndipo ulipozuka ugomvi. “Inadaiwa kuwa baada ya mume huyo kuja saa moja mke alimuhoji kwa nini amechelewa kurudi ndipo ugomvi ulipoanza ambao unaelezewa ni wivu wa
kimapenzi na hatimaye mke kumchoma kisu mumewe na kufa papohapo,” alisema.
Aidha kamanda alisema mwanamke huyo anashikiliwa na polisi na kwamba atafikishwa mahakamani wakati wowote uchunguzi utakapokamilika.
Katika tukio la lingine mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Lucia Thadeus Shirima amefariki dunia na mwingine kujeruhiwa baada ya gari alilokuwa akisafiria lenye namba T 984 BCT, aina ya Scania mali ya Kampuni ya Saibaba, kugongana uso kwa uso na gari aina ya Toyota Hice namba T 465 APZ.
Kamanda Boaz alisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Mgagao wilaya ya Mwanga Barabara kuu ya Moshi-Tanga, majira ya saa saba na nusu mchana, wakati basi hilo likitokea Jijini Arusha kuelekea jijini Dar es salaam na Toyota Hice ikitokea jijii Dar es salaam kuelekea Arusha.
Kamanda alimtaja aliyejeruhiwa kuwa ni dereva wa Toyota hice Thadeus Shirima (38) ambaye amelazwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC kwa ajili ya matibabu ambapo na kwamba aliyefariki ni mke wa dereva huyo. Kamanda Boz alisema chanzo cha ajali hiyoni ni uzembe wa Dereva wa
Toyota Hice kulipita gari lililokuwa mbele yake katika eneo ambalo haliruhusiwi ndipo alipokutana uso kwa uso na basi la Saibaba.
Wakati huohuo mtu mmoja ambaye ni mwanamume mwenye umri kati ya miaka 30 na 35 ameokotwa akiwa amekufa katika eneo la barabara ya Tifa mjini Moshi pembeni na kanisa katoliki la Kristu Mfalme. Kamanda Boaz alisema maiti ya mtu huyo iliyoifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi ilipopekuliwa ilikutwa na kifaa cha kufungulia vivywaji (opena) na karatasi iliyokuwa na bili ya vinywaji. Maiti hiyo bado hijatambuliwa.