Mkataba wa Kuleta Amani Kongo Watiwa Saini Ethiopia

Matumaini ya kumalizika maapigano Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

MKATABA wa kumaliza vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo leo umetiwa saini mjini Addis Ababa-Ethiopia na viongozi wa nchi za Maziwa Makuu. Viongozi wa nchi za maziwa makuu leo mjini Addis Ababa wameutia saini mkataba wa kumaliza vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo uliofikiwa kwa upatanishi wa Umoja wa Mataifa.

Viongozi hao walishindwa kuutia saini mkataba huo mwezi uliopita kutokana na mzozo juu ya nani anapaswa kukiongoza kikosi cha kulinda amani kitakachowekwa mashariki mwa Jamhuri ya Kongo.

Kutiwa saini kwa mkataba huo kutawezesha kuundwa kwa kikosi maalum cha jeshi la Umoja wa Mataifa kitakachoweza kuingilia kati katika eneo hilo la mashariki mwa Kongo na kupambana na waasi pamoja na kuanzisha juhudi mpya za kisiasa. Viongozi walioutia saini mkataba huo mjini Addis Ababa ni wa Msumbiji, Rwanda, Tanzania, Afrika Kusini, Kongo, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Sudan ya Kusini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Nesirky ameeleza kuwa Umoja wa Afrika, mataifa 11 ya eneo la maziwa makuu, (ICGLR)pamoja na jumuiya ya wanachama 14 ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika SADC,watakuwa “wadhamini wenza”.

Umoja wa Mataifa unatarajiwa kumteua mjumbe maalum atakaefuatilia utekelezaji wa makubaliano hayo. Maofisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa hali ya kutokubaliana mwezi Januari ilitokana na wasi wasi juu ya taratibu, lakini sio kutokana na maudhui ya mkataba. Jason Stearns, mchambuzi anaefuatilia masualaya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, mapema mwezi huu aliyaita makubaliano hayo kuwa ni “hati isioeleweka kabisa.”

Amesema makubaliano hayo, yanalenga katika vipengere vitatu:”kuyazuwia mataifa ya eneo husika kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi nyingine, kuhimiza kufanyiwa mageuzi kwa taasisi dhaifu nchini Kongo na kuvutia uratibu bora zaidi wa wafadhili na ushiriki wao.

Eneo la mashariki mwa Kongo ambalo lina utajiri mkubwa wa madini limevurugwa na makundi kadhaa yenye silaha katika muda wa miongo miwili iliyopita, huku makundi mapya ya waasi yakizuka kila mara, baadhi yao yakiungwa mkono na nchi jirani.

Ongezeko la hivi karibuni la machafuko lilitokea mwaka 2012 na kusababisha kuzuka kwa kundi la waasi la Machi 23, (M23) ambalo kwa muda liliuteka mji muhimu wa Goma Novemba mwaka jana. Kundi la M23 liliundwa na wapiganaji wa zamani wa kundi la waasi wa kabila la Watutsi ambao hapo awali waliingizwa katika jeshi rasmi la Serikali ya Congo kwa mujibu wa makubaliano ya amani, lakini wanadai kuwa masharti ya makubaliano hayo hayakutimizwa.