Mkapa kuanza mashambulizi Igunga leo

Rais mstaafu Benjamin Mkapa (kulia) akisalimiana na Mgombea Ubunge wa CCM Igunga, Dk. Peter Kafumu

Na Bashir Nkoromo, Igunga

MWENYEKITI mstaafu wa CCM, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa anaunguruma leo mjini hapa atakapohutubia mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM za uchaguzi mdogo jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Msimamizi wa shughuli za uchaguzi za CCM, Matson Chizi alisema jana kwamba mkutano huo utafanyika kwenye Viwanja vya kumbukumbu ya Sokoine katikati ya mji huo mdogo wa Mpanda. Viwanja hivyo ndivyo CHADEMA pia walitumia kufanya mkutano wao wa uzinduzi wa kampeni zao juzi.

“Maandalizi yamekamilika na tumepanga kuufanya mkutano huu kuwa wa aina yake ili kuonyesha uwezo na nguvu ambazo Chama Cha Mapinduzi kinazo katika jimbo hili na mkoa wa Tabora kwa jumla,” alisema Chizi.

Alisema mkutano huo utaweza kuonyesha kuvu halisi za Chama ikizingatiwa kwamba wabunge wote Tabora ni wa CCM na katika jimbo la Igunga linalogombewa sasa katika uchaguzi huo CCM ina madiwani 32.

“Ukitazama mtandao huu wa kiuongozi na idadi kubwa ya wanachama tulio nao jimboni mkutano wetu utakuwa mkubwa sana na tunatarajia utaweka historia Igunga,” alisema Chizi.

Mkapa ambaye aliwasili juzi, mjini hapa, jana alikuwa na mikutano ya ndani ya CCM ambapo alikutana na viongozi wa ngazi mbalimbali na kufanya mikakati halali itakayokiwezesha Chama Cha Mapinduzi kuibuka na ushindi.

Wakati CCM inazindua kampeni zake leo, kampeni kwa vyama vyote vinavyoshiriki ucjaguzi jimbo hapa zilianza arasmi Septemba 7, mwaka huu na zitadumu hadi Oktoba 2, mwaka huu uchaguzi utakapofanyika.

Jumla ya vyama vinane vimeweka wagombea katika uchaguzi huo ambapo mbali na CCM vimo CUF, UPDP,CHAUSTA, AFP,CHADEMA,DP na SAU. Uchaguzi huo unafanyika kufuatia aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo la Igunga, Rostam Aziz kujiuzulu kutokana na sababu za kisiasa.