Mkapa awekwa `kiti moto` UDSM

Rais Mstaafu, Mh. Benjamin Mkapa

Mzimu wa ubinafsishaji uliofanywa dhidi ya yaliyokuwa mashirika ya umma, unazidi kumuandamana Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ingawa binafsi bado hajaona athari zake.

Kwenye siku ya mwisho wa kongamano la nne la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) sehemu ya Mlimani jana, wanazuoni na wadau wengine, walimshambulia kwa kumkosoa Mkapa kuhusu ubinafasishaji uliofanywa wakati wa utawala wake.

Lakini Mkapa aliyeonekana ‘kupandwa na jazba’ wakati akijibu hoja za wanazuoni, alizidi kuutetea ubinafsishaji huku akisema lengo kuu lilikuwa kuyaondoa mashirika na viwanda vya umma katika utawala uliokuwa mbovu.

Dk. Mwanza Kamata alikuwa ‘mchokonoaji’ wa kwanza kuhusu udhaifu uliobainika katika ubinafsishaji na kumuita Mkapa kuwa ‘shahidi na mfunguaji’ wa bidhaa kutoka nje kupitia ubinafsishaji.

Hata hivyo, Mkapa alisema ubinafsishaji haukufanyika kwa lengo la kuingiza bidhaa za nje, bali kuviokoa viwanda na mashirika ya umma aliyosema yalikuwa mufilisi.

Alisema kama viwanda na mashirika yaliyobinafsishwa vilirejea kile alichokiita kuwa ‘utumbo ule ule’, haliwezi kuwa kosa lake akiwa Rais wa awamu ya tatu, lakini hakumtaja anayelistahili kosa hilo.

Mkapa alisema ujenzi wa uchumi unahitaji soko, mitaji na utawala ambao hata hivyo alizidi kusisitiza kuwa kwa mashirika na viwanda vya ndani (utawala) wake ulikuwa wa hovyo.

Mkapa alisema akiwa Rais wa awamu ya tatu, serikali yake ilibinafsisha viwanda na mashirika ya umma yanayofikia 330, miongoni mwa hayo 180 yakikabidhiwa kwa wazawa, 23 kwa raia wa kigeni na yaliyobaki yakaendeshwa kwa ubia.

“Fanyenyi utafiti ili kujua miongoni mwa hayo yaliyoendeshwa vizuri ni yapi na yaliyobaki kuwa ya hovyo ni mangapi, tafuteni na sababu zake kwamba yalikuwa makosa ya nani, kisha tutarekebishaje,”alisema.

Mkapa alisema kwa taarifa alizonazo, ubinafsishaji umeleta mafanikio makubwa kwa nchi na kwamba anashangazwa na lawama na laana zinazotolewa na wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema ubinafsishaji uliofanyika wakati wa utawala wa Mkapa, uliathiri hadi sekta muhimu za mikakati ya kiuchumi, hivyo kulifanya taifa lishindwe kuudhibiti uchumi wake.

Profesa Shivji alisema ubinafsishaji kwa nia ya kuwekeza, ulifanyika hata kwa nchi kama China na Vietnam, lakini tofauti na Tanzania mataifa hayo yalihusisha sekta zisizoathiri udhibiti wa uchumi wao.

Alipendekeza kuwepo uthubutu wa viongozi kukataa masharti ya mataifa ya nje hususani ya Ulaya na Marekani, yanapobainika kuwa na masharti yanayoathiri uchumi wa nchi.

Hata hivyo, Mkapa alisema kabla ya kuthubutu kusema hapana kwa mataifa hayo, lazima umma ujiulize ikiwa utathubutu kuhimili changamoto zitakazotokana na kuyatamkia mataifa hayo hapana kwa mashari yao.

Mkongwe wa tasnia ya habari nchini, Jenerali Ulimwengu alisema uwezo wa kusema hapana utawezekana ikiwa viongozi watajivua hadhi ya utawala na kurejea kwa wananchi, wakipanga mipango yenye lengo la kuushirikisha umma kumiliki uchumi wa nchi.

Kwa upande mwingine baadhi ya wanazuoni waliochangia kwa nyakati tofauti, walisema wakati umefika kwa umma kusema ‘hapana’ dhidi ya watawala.

Walisema hali hiyo inapaswa kuchukuliwa kupitia sanduku la kura kwa kuwachagua viongozi wenye maono na nia njema za kuingoza nchi, ili ipige hatua stahiki kiuchumi na kijamii.

CHANZO: NIPASHE