Mkapa asema viwanda ni muhimu kwa maendeleo ya EAC

Rais mstaafu wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nchi za Kusini

Na Nicodemus Ikonko, EANA

RAIS mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Benjamin Mkapa, amesema kwamba iwapo Afrika Mashariki imepania kuleta maendeleo katika kanda hiyo, haina budi kukuza viwanda na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Mkapa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Nchi za Kusini, iliyoasisiwa na Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, amezitaje njia nyingine za kuleta maendeleo katika kanda hiyo kuwa ni pamoja na kuongeza uweze wa ndani wa uzalishaji.

“Hakuna njia nyingine mbadala ya kujiletea maendeleo ya uhakika na la muhimu zaidi ni kuongeza ajira na usalama wa chakula. Hatuwezi kuendelea kuuza nje kiasi kidogo cha bidhaa zetu na kuagiza kiwango kikubwa cha bidhaa zilizozalishwa nje katika harakati za kujiletea maendeleo,” alisisitiza.

Mkapa alikuwa anatoa hutoba ya ufunguzi katika warsha ya siku tatu kuhusu majukumu ya makubaliano ya mashirika ya biashara ya kimataifa katika kuhimiza maendeleo na biashara Afrika kwa kushirikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) katika majadiliano na Shirika la Biashara Duniani (WTO) na Makubaliano ya Ubia wa Uchumi wa Umoja wa Ulaya (EPA).

“Ni asilimia sita tu ya bizaa zetu tunazouza EU(Umoja wa Ulaya) zimeongezewa thamani kwenye viwanda vyetu wakati asilimia 94 inayobaki huuzwa kwenye soko hilo kama malighafi,” alieleza.

Alionya kwamba iwapo kanda ya EAC itakubali kuingia makubaliano na EPA na kanda nyingine za kiuchumi Afrika pia zikafanya hivyo, zitakuwa zimeacha njia bora zaidi ya kujiletea maendeleo, ambayo ni ile inayoruhusu uanzishwaji wa viwanda vya uhakika badala ya kuendelea kuuza nje ya nchi mazao ghafi. Katika hili Mkapa alieleza kwa uhakika kwa kusema “kazi ngumu ya kuanzisha viwanda and uzalishaji wa chakula haina budi kutekelezwa.”

Alijiuliza swali juu ya dhamira halisi ya EPA kwa kusema;” Hivi EPA inaingia katika majadiliano kwa sababu inajali Afrika na ushirikiano wa EAC na maendeleo? Au imesukumwa tu kwa msingi na matakwa yao ya kiuchumi?

Alisema Umoja wa Ulaya (EU) kama wabia wa Afrika katika maendeleo ina lengo maalum katika majadilaino yanayoendeshwa na EPA hususan ni “mahitaji ya kidiplomasia ya malighafi inayoambatanishwa na sera za kukuza haki za binadamu, utawala bora na mengineyo…”.

Alisisitiza kwamba makubaliano yoyote ya kibiashara na taasisi za kimataifa hayana budi kuleta manufaa kwa EAC na hivyo kila awamu ya majadiliano ni lazima ichunguzwe kwa makini, Shirika la Huru la Habarai la Afrika Mashariki (EANA) limeripoti

Awali akimkaribisha Mkapa kutoa hotuba yake ya kuu ya ufunguzi wa warsha hiyo, Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Richard Sazibera alisema kuna haja ya kuwa na ubia endelevu ambapo pande zote zinazohusika katika majadiliano hazina budi kunufaika.

Warsha hiyo inajumisha watu na taasisi mbalimbali ikiwa ni pomoja na makatibu wakuu wanaohusika na masuala ya biashara na EAC, wawakilishi toka sekretarieti ya Afrika, Visiwa vya Caribbian na Pasifiki, mabalozi wa nchi wanachama wa EAC waliopo Ubelgiji na Geneza,Uswisi, wabunge wa mabunge ya kitaifa na wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), sekta binafsi na makundi ya kiraia.

Wajumbe wa warsha hiyo pamoja na mambo mengine watajadili uhusianowa WTO na EPA katika kushirikisha EAC kwenye majadiliano na mashirika hayo mawili ya dunia kuleta manufaa kwa kanda hiyo ya Afrika.