Na Mwandishi Wetu, Tanga
MJUMBE wa Baraza Kuu la Taifa la Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko amefunga tawi la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Kijiji Cha Lukozi na kupandisha Bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika tawi hilo na kutangaza ufalme mpya wa Chama hicho cha siasa eneo hilo.
Tukio hilo limetokea Machi 6, 2014 katika Kijiji cha Lukozi, wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga, ambapo sambamba na kuasisi tawi hilo la CCM pia kiongozi huyo wa UVCCM alifanikiwa kuwaingiza wanachama wapya 206 ambapo wengi wao walikuwa ni wanachama wa CHADEMA.
Mjumbe huyo wa Baraza Kuu la Taifa la UVCCM, pia alifungua mashina sita yakiwemo ya Manyara, bodaboda na pia kufanya vikao vinne vya ndani ambapo alizungumza na wanaCCM juu ya hali ya Uimara wa Chama na kuhoji kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika Kijiji hicho ndani ya Wilaya ya Lushoto pamoja na kufanya mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na wananchi wengi wa Lukozi.
Pamoja na vikao hivyo lakini pia Husna alitembelea vikundi vya ujasiriamali vya akinamama pamoja na kambi ya JUDO ya Vijana wilayani Lushoto na kujadili nao Changamoto wanazokutana nao na kushirikiana nao kuzipatia ufumbuzi.
Husna anafanya ziara za kawaida katika Mkoa mzima wa Tanga katika kuhamasisha Vijana kujiunga na Chama Cha Mapinduzi pamoja na Jumuiya ya Umoja wa Vijana.