Mhindi (pichani) aliyefahamika kwa jina la Abdulla Punathil Usman amepatikana akiwa mgonjwa hospitalini, nchini Dubai. Usman hakuwa na mawasiliano na familia yake na wala hawakuwa na habari zake tokea asafiri kwenda Dubai miaka ya 70.
Akiwa na umri zaidi ya miaka 60 sasa, rafiki zake wa Dubai walianza kuwatafuta ndugu zake huko India baada ya Usman kulazwa hospitalini akisumbuliwa na donda kubwa mguuni, ambalo amekuwa akisota nalo kwa takribani miezi miwili kabla ya kufikishwa hospitali mwezi huu. Rafiki wa Usman aliyefahamika kwa jina la Abdul Gafoor, ambaye anajishughulisha na udereva mjini Dubai, alisema kuwa Usman alikuwa anafanya kazi kama mpishi kwenye nyumba ya Muarabu tokea alipofika nchini humo kutokea kijijini kwake Chakkavad, India.
Baada ya Gafoor kusambaza habari za Usman kwenye vyombo vya habari, alianza kupokea simu nyingi kutoka kwa watu waliopo India na Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE), lakini wengi hawakuweza kumtambua Usman. Hatimae, Bw. Haneefa, ambaye anajishughulisha na udereva pia nchini Dubai na akiwa ametokea kijiji cha Chakkavad, India, aliweza kumtambua Usman kama mjomba wake aliyepotelea Dubai miaka mingi iliyopita! Haneefa alisema baada ya kusoma habari za Usman alishtushwa na jina lake na sehemu anayotoka India (Chakkavad), hivyo basi kutaka kujua zaidi. Bw. Haneefa aliongeza kusema “Machale yalinicheza, nakumbuka wakati nipo shule, mmoja wa makaka wa mama, alisafiri kwenda Ghuba (Gulf), bila kurudi, na hakukuwa na taarifa zozote kuhusu maendeleo yake. Nilishikwa na hamasa kubwa ya kutaka kukutana na mtu huyu.”
Haneefa alienda hospitalini kukutana na Usman, na baada ya mazungumzo mafupi aliweza kugundua kuwa jamaa ndie haswa Yule mjomba wake aliyetoweka miaka 40 iliyopita, ingawa sasa sio yule mjomba wake kijana aliyemfahamu, kwani Usman amezeeka na kudhoofika. Pamoja na hayo, Usman bado aliweza kujibu maswali yote aliyoulizwa na Haneefa kuhusu familia yao huko Chakkavad, India. Swali gumu pengine kuliko yote kwa Usman, lilikuwa ni kwanini aliamua kukaa kimnya (bila mawasiliano na familia yake) kwa muda wote huo aliokaa Dubai? Usman alijibu tu kwa ufupi kwamba “Hamna kitu, ni muda tu umepita.” Usman anaendelea vizuri na matibabu na ataruhusiwa kutoka hivi karibuni baada ya deni la matibabu yake, ambalo limefikia Dirham 18,040 (ambalo ni takriban TSH 8,415,883.76) kulipwa.
Ingawa Usman hana mtoto wala familia kwa miaka yote aliyokaa Dubai, anasifika kwa uaminifu na uadilifu wake katika kazi. Visa yake ya kuishi Dubai itakwisha (expire) Novemba 15 mwaka huu, na familia yake aliyopoteana nayo miaka yote hiyo, inatarajia kumpokea atakaporudishwa nchi India. Ubalozi wa India nchini Dubai umeonyesha nia ya kugharamia safari ya Usman kuelekea India. Usman pia anafuraha ya kwenda kuonana na familia yake huko India, lakini alipoulizwa endapo angependa kurudi Dubai, alisema “Hamna ajuae, lolote litakalo kuwa, lita kuwa.”
Ndugu zangu wa Ughaibuni tunajifunza nini kutoka kwenye habari hii?
Chanzo: Yahoo News: https://en-maktoob.news.yahoo.com/missing-indian-found-family-40-years-055015916.html
Imetafsiriwa na dev.kisakuzi.com