Mjini Magharibi yatinga 16 bora

Logo ya Michuano ya Copa Coca Cola

*Wachezaji 11 wamaliza mikataba Coastal Union

MJINI Magharibi imetinga hatua ya 16 bora ya michuano ya Copa Coca-Cola baada ya Julai 4 mwaka huu kuilaza Tanga bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Bao la washindi katika mechi hiyo ya kundi B lilifungwa dakika ya 68 na Juma Ally. Kwa matokeo hayo Mjini Magharibi ambayo imemalizika mechi zake imefikisha pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine katika kundi hilo.

Mbeya imejipatia ushindi wa pili mfululizo katika kundi lake la C baada ya leo kuifunga Mara bao 1-0 katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam. Mshambuliaji John Jerome alifunga bao hilo pekee dakika ya 43.

Licha ya ushindi huo Mbeya wameshindwa kukata tiketi ya 16 bora kwani wamemaliza mechi zao wakiwa na pointi sita tu. Timu za Dodoma yenye pointi 12 na Kinondoni ambayo imefikisha pointi 10 na mechi moja mkononi ndizo zilizofuzu kucheza 16 bora kutoka kundi hilo.

Pwani imepata ushindi wake wa kwanza katika kundi lake la D baada ya leo kuichapa Kagera mabao 3-1 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Cotiveno Ngaga dakika ya 19, Abdallah Juma dakika ya 30 na Salum Ame dakika ya 68.

Kagera ambayo imebakiza mechi moja dhidi ya Shinyanga ikiwa na pointi sita ilipata bao dakika ya 42 kupitia kwa Athuman Kassim. Nazo Ruvuma na Arusha zimetoka suluhu katika mechi ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Tamco.

Wakati huo huo; WACHEZAJI 11 wamemaliza mikataba yao ya kuichezea timu ya Coastal Union ya Tanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, na sasa wako huru kujiunga na klabu yoyote.

Kwa mujibu wa Coastal Union, wachezaji hao ni Ben Mwalala, Samwel Temu, Francis Busungu, Ahmed Shiboli, Lawrence Mugia, Daudi Chengula, Godfrey Mmasa, Mwinyi Abdulrahman, Sabri Ramadhan China, Soud Abdallah na Ramadhan Wasso.

Uhamisho wa wachezaji kwa msimu huu ulianza Juni 15 mwaka huu na utamalizika Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuanza wachezaji (kwa wasio wa Ligi Kuu) ni kati ya Juni 15 na 30 mwaka huu.

Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.