KAULI aliyoitoa leo mwandishi na mmiliki wa Mjengwa Blog inaonesha Jeshi la Polisi limemjumuisha kuwa miongoni mwa watuhumiwa wanaodaiwa kumshambulia, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.
“Leo nilifika tena Makao Makuu ya Jeshi la Polisi. Nilikutana na Kamishna wa Polisi ( Upelelezi) Advocate Nyombi na Ofisa mwingine wa Idara hiyo. Kamishna Nyombi alinijulisha kuwa uchunguzi wa suala la Kibanda ungali ukiendelea. Nami nabaki kwenye kundi la watuhumiwa; tuhuma za kumjeruhi Absalom Kibanda.
Tumekubaliana nifike tena Makao Makuu ya Polisi Aprili 23. Ahsanteni sana kwa kuendelea kunifariji kwenye kadhia hii iliyonikuta. Na hakika, nawashukuru sana kwa kuendelea kuniamini. Ni dhahiri, kuwa kweli itakuja kudhihiri, hata kama kweli hiyo itachelewa kutufikia. Na tuwe wenye subira.” Hii ni kauli ya Maggid Mjengwa aliyoitoa leo Dar es Salaam kupitia mtandao wake (Mjengwa Blog).