Na Joachim Mushi
BAADHI ya wanaharakati wamevitaka vyombo vinavyotunga sheria nchini kwa pamoja kwa kushirikiana na wanaharakati kuhakikisha wanashinikiza kutungwa kwa sheria itakayo simamia bajeti za kila mwaka na pale ambapo Serikali na idara fulani zinaonekana kukwamisha utekelezaji sheria ichukue mkondo wake.
Kauli hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es Salaam na baadhi ya wawakilishi kutoka asasi anuai za kiraia ambao walishiriki katika mjadala wa wazi wa kudai uwajibikaji kwa watunga sera kwa kuzingatia mgawanyo wa rasilimali kijinsia ulioandaliwa na TGNP Mtandao.
Akizungumza katika majadiliano mwakilishi wa wa asasi ya Network for Vulnerables Rescue Foundation (NVRF), Ezekiel William alisema anakerwa na kitendo cha serikali kupanga bajeti kila mwaka lakini asilimia kubwa ya fedha za bajeti hasa zile za maendeleo hazipelekwi katika wizara na idara kama ilivyopangwa.
“…Mimi ni miongoni mwa watu wanaokerwa na kitendo cha Serikali kupanga bajeti na bunge kuidhinisha lakini baadaye unasikia idara na wizara zikilalamika kuwa asilimia 45 ya bajeti ya bajeti zao haikupelekwa hivyo haikutekelezwa hadi muda unaisha…mwaka mwingine inatengwa nyingine na mambo ni yaleyale,” alisema William.
“…Kuna haja ya kutungwa sheria ya kusimamia bajeti, yaani endapo bajeti haijatekelezwa sheria ichukuwe mkondo wake…washtakiwe wale waliokwamisha utekelezaji wa bajeti hiyo hii itakuwa ni fundisho na itachochea maendeleo,” alisisitiza William.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SIKIKA, Irenei Kiria akiwasilisha mada juu ya huduma zinazotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na changamoto zake, alisema bado sekta hiyo inachangamoto nyingi kwani uhaha wa vitendea kazi wataalamu katika maeneo mbalimbali ya wizara ni takribani asilimia 50 licha ya bajeti ndogo inayopangwa kila mwaka.
Naye Ofisa Miradi wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), Bi. Asha Komba akiwasilisha mada yake juu ya rushwa ya ngono nchini‘Sextortion’ alisema matokeo ya rushwa hiyo yamekuwa na madhara makubwa kiutendaji jambo ambalo alishauri asasi mbalimbali kuungana kukabiliana nayo kwa kuhamasisha utoaji taarifa.
Alisema rushwa ya ngono imekwamisha utendaji kazi na usimamizi maeneo mbalimbali ndani ya Serikali na nje katika asasi na taasisi anuai jambo ambalo linakwamisha maendeleo nchini na unyanyasaji wa kijinsia.
Aidha alisema kuongezeka kwa rushwa za ngono zimeongeza migogoro katika familia na kuathiri maendeleo ya elimu katika ngazi zote za elimu, pia alitolea mfano kwamba kuongezeka kwa idadi ya wasichana wanaofeli kunachangiwa na rushwa za ngono. “…Rushwa za ngono zimeongeza mimba utotoni, zimechangia kushuka kwa viwango vya elimu na sasa ni kikwazo katika elimu ya vyuo,” alisema Bi. Komba.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya ambaye aliongoza mjadala huo ulioshirikisha asasi anuai kutoka Dar es Salaam na mikoa ya jirani ikiwemo Pwani na Morogoro, aliwataka washiriki kuhakikisha wanaunganisha nguvu zao na kupaza sauti kusimamia hoja za msingi wanazo ziibua kwa manufaa ya jamii kwa kuzingatia makundi yote.