RAIS wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema kuwa hana wasiwasi na hali ya mjadala mkali uliotawala Bunge Maalum la Katiba kwa sababu ni muhimu kwa mjadala kuhusu Katiba Mpya ukawa wa kina ili kuweza kupata Katiba bora kwa Watanzania. Rais Kikwete alisema kuwa Katiba ya Tanzania haitapatikana kwa mikutano ya kisiasa nje ya Bunge Maalum la Katiba bali ndani ya Bunge hilo ambako ni dhahiri kuwa mjadala utatawaliwa na nguvu ya hoja na busara.
Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ametoa ufafanuzi huo Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College – kilichoko Kunduchi, Dar es Salaam.
Wakati wa kipindi cha maswali na majibu, ofisa mmoja wa Jeshi la Kenya alimwuuliza Rais Kikwete kama alikuwa na wasiwasi kuhusu mjadala unaoendelea nchini kuhusu Katiba Mpya unaweza kuvuruga usalama wa Tanzania. Rais Kikwete amemjibu: “Sina wasiwasi hata kidogo kwa sababu hatukutarajia kuwa mjadala wa Bunge Maalum la Katiba kuhusu jambo hili kubwa ungekuwa rahisi. Yalipojitokeza maoni ya Tanzania kupata Katiba Mpya, tuliunda Tume na tume hiyo ikatoa ripoti yake ambayo ndiyo inajadiliwa katika Bunge Maalum. Hatukutarajia kuwa mjadala kuhusu ripoti ungekuwa rahisi kwa wajumbe kutoa majibu ya ndiyo ama hapana.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea ni jambo muhimu na la lazima…najua wakati mwingine majadiliano yalikuwa makali mno lakini hili ni jambo zuri. Aina ya mfumo na muundo wa Serikali lilizusha mjadala mkali lakini hayo ni matokeo ya hali halisi ya masuala yanayojadiliwa.”
“Ni imani yangu kuwa tutafikia mwisho. Mwisho upi, hilo ni suala la Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kuamua. Muhimu ni kwamba Katiba Mpya inaweza kupatikana kutoka Bungeni tu siyo kupitia mikutano ya hadhara nje ya Bunge. Huko hakuna Katiba huko kuna mikutano ya hadhara na siasa tu. Katiba itapatikana kwa mijadala na kwa nguvu ya hoja ndani ya Bunge letu.”
JK: Vyama vingi vimepanua wigo wa kisiasa
Wakati huo huo, Rais Kikwete amesema kuwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ni mzuri, umeleta matumaini kwa kupanua wigo na kufungua zaidi uwanja wa kisiasa pamoja na kuiwajibisha Serikali.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa ili mfumo huo uboreshwe zaidi na uweze kuimarisha misingi mikuu ya maendeleo ni lazima uendeshwa kwa watu kufuata sheria na wala siyo kuingiza matumizi ya nguvu ambayo yanaweza kuvuruga nchi.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la mwanafunzi wa kozi ya pili kwenye chuo hicho kutoka Kenya ambaye alitaka kujua jinsi gani vyama vingi vya siasa vinavyoathiri umoja wa kitaifa na kuibadilishaTanzania kufuatia miaka zaidi ya 30 ya Tanzania kuwa nchi yenye kuleta matumaini kwa nchi nyingine za Afrika na Waafrika.
“Vyama vingi ni vizuri. Mfumo wa vyama vingi unaleta matumaini kwa kupanua wigo wa kisiasa ambao haukuwa mpana kiasi hicho huko nyuma. Sasa mtu anaweza kuamua kujiunga na chama chochote cha siasa anachokipenda yeye,” alisema Kikwete.
Aliongeza rais Kikwete: “Ni mfumo ambao unaiwajibisha Serikali. Ni mfumo mzuri kwa upanuzi wa demokrasia. Sasa watu wanaweza hata kuamua kupunguza bajeti ya safari za Rais nje ya nchi. Wanadhani kuwa Rais anaweza kufanikiwa zaidi na Tanzania kupita hatua za maendeleo haraka zaidi kama Rais atabakia amejifungia ndani ya nchi.”
“Jambo la maana ni kwamba tunahitaji aina mbali mbali ya mawazo. Mawazo ya namna hiyo hayaathiri demokrasia. Mawazo ya namna hiyo yanasaidia hata chama changu kuimarika zaidi.”
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa mfumo huo utavurugika endapo baadhi ya watu wataendekeza matumizi ya nguvu na hoja za nguvu badala ya kupambana kwa hoja na nguvu ya hoja.
“Wasiwasi wangu ni kuingiza matumizi ya nguvu katika ujenzi wa demokrasia. Ni makosa kwa watu kukimbilia kutumia nguvu baada ya kushindwa kwenye hoja. Na hili halivumiliki na likitokea basi Serikali itaingilia kati kudumisha amani.”