Na Edwin Moshi, Makete
HIFADHI ya taifa ya Kitulo iliyopo wilayani Makete mkoani Njombe imejipanga vilivyo kuongeza vivutio vipya vya utalii hifadhini humo pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara na njia za kupita watalii ili wafurahie vivutio vilivyopo hifadhini humo.
Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Makete iliyofanya ziara hifadhini humo, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Kitulo, Pius Mzimbe alisema hivi sasa wanazidi kuboresha hifadhi hiyo ambapo kwa mwaka wa fedha 2014/15 wataboresha barabara za hifadhi hiyo ili kusaidia kufikika kirahisi kwa vivutio lukuki vinavyopatikana kwenye hifadhi hiyo hasa kwenye maporomoko ya maji pamoja na kujionea mimea ya aina mbalimbali iliyoota kwenye hifadhi hiyo.
“Kwa mfano kwa sasa tunajenga camp site (vituo vya kupumzikia watalii) ambapo watalii wakiwa hapa watajionea mandhari mabalimbali ikiwemo milima, mimea na vingine, watapanda kwenye milima na kuona maeneo ya mbali na wakichoka watarudi hapa kupumzika na tutawawekea bafu na maliwato kwa ajili yao pamoja na jiko kwa ajili ya kuwapikia vyakula wanavyovipenda hasa vya asili” alisema Mzimbe.
Amesema kumekuwa na changamoto ya kutofikia baadhi ya vivutio hasa maporomoko ya maji kutokana na ubovu wa barabara wakati wa masika hivyo kwa kuziboresha kutasaidia barabara hizo kupitika muda wote hivyo kuongeza mapato yatokanayo na hifadhi hiyo ya Kitulo.
Bw. Mzimbe ametoa wito kwa wananchi wa ndani na nje ya Makete kujijengea utaratibu wa kutembelea hifadhi hiyo ili wajionee vivutio mbalimbali ikiwemo maua, ndege, maporomoko ya maji na mimea mbalimbali ambayo ipo hifadhini humo tu na vivutio vingine ambavyo wanavigundua siku hadi siku.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Makete ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya, Josephine Matiro amesema wilaya yake imebarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya kitalii ambavyo vipo ndani ya hifadhi ya Kitulo na vingine vipo nje hivyo wao kama serikali watahakikisha vivutio hivyo vinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha baadaye.
Matiro amesema ni vyema wanamakete wakajitokeza kwa wingi kufanya utalii wa ndani na kujionea jinsi wilaya yao ilivyobarikiwa na ni jambo la aibu kwa watalii wa nje ya nchi kuja kutembelea hifadhi ya Kitulo ilihali wakazi wa makete hawajawahi kuitembelea.
“Kwa mfano leo tumejionea vivutio vingi humu hifadhini, lakini ukipita kwa gari unaishia kuona maua ama ndege lakini ukiingia humu ndani vipo vivutio vingi vya ajabu na vya kuvutia, mimi na kamati ya ulinzi na usalama tumeamua kuonesha mfano, tunaomba wananchi mtuunge mkono kwa kuja kuitembelea hifadhi yetu ya kitulo,” alisema Matiro.
Wakiwa hifadhini humo wajumbe wametembelea maporomoko ya maji ya Mwakipembo na Numbwe ambayo ni marefu zaidi, pamoja na eneo ambalo linajengwa vituo vya kupumzikia watalii na pia kujione mandhari tulivu ya hifadhi hiyo ya Kitulo. Hifadhi ya Kitulo ipo katika tarafa ya matamba wilayani Makete na inasifika duniani kwa kuwa na maua na ndege na kwa hivi sasa vivutio vingine vya utalii vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku.