Miti 120 yavunywa kinyemela Moshi

uharibifu na uvunaji wa misitu unaofanywa kinyemera

Na mwandhishi wetu-Kilimanjaro
LICHA ya serikali mkoani Kilimanjaro kupiga marufuku uvunaji wa miti kwa lengo la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,watu wasio fahamika wamevuna miti ya asili aina ya mikuyu 120 katika mtaa wa matindigani kata ya Pasua manispaa ya Moshi jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Watu hao wanadaiwa kuwa walikata miti hiyo kwa lengo la kuendeleza ujenzi katika eneo hilo pasipo kufuata sheria na taratibu za halmashauri ya manispaa ya Moshi za kuomba vibali.
Kufuatia tukio hilo mkurugenzi wa manispaa ya moshi Bi. Bernadette Kinabo alilazimika kufika katika eneo la tukio ili kujionea hali halisi ambapo aliwakuta baadhi ya vijana wakiendelea na shughuli za ujenzi na vijana hao kueleza kuwa hawahusiki na tukio hilo na kwamba wao ni vibarua.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa Bi.Kinabo alisema kitendo cha uvunaji miti mingi kiasi hicho kwa wakati mmoja ni cha kinyama kutokana na kwamba kinachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo kwa athari za mabadiliko ya Tabianchi.
“Kwa sasa katika mkoa wetu tumeanza kampeni ya kuotesha miti ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yametuathiri kwa kiasi kikubwa, na sasa yamesababisha katika mji wa moshi kuingia katika mgao wa maji kwa mara ya kwanza,lakini vitendo hivi vinavyoendelea vya ukataji miti kwa kweli vinarudisha nyuma jitihada zetu”alisema Bi. Kinabo.
Aidha Bi. Kinabo alisema halmashauri hiyo haitokubali kuvifumbia macho vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kuhifadhi na kulinda mazingira na kwamba wote waliohusika watachukuliwa hatua za kisheria ili kuweza kudhibiti vitendo hivyo.
Baada ya mkurugenzi kutembelea eneo la tukio akifuatana na mwanasheria wa manispaa na afisa mipango miji , alifika katika kituo cha polisi kutoa taarifa ambapo polisi walifika eneo la tukio na kuwakamata vijana watano waliokuwemo katika eneo hilo.
Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro Bw. Robert Bioaz alithibitisha kukamatwa kwa vijana watano na kusema kuwa vijana hao wanashikiliwa kwa mahojiano na kwamba uchunguzi zaidi bado unaendelea ili kuweza kuwabaini wahusika wa tukio hilo na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Tukio hilo limetokea ikiwa zimebaki siku chache ili kuadhimisha wiki ya mazingira ambayo inatarajiwa kuanza Jun tatu hadi Juni Tano mwaka huu na kitaifa inafanyikia mkoani Kilimanjaro.