KIZUNGUMKUTI kilichotanda tangu kutangazwa kwa mshindi wa taji la Miss Tanzania 2014, Sitti Abbas Zuberi Mtemvu leo kimeingia katika utata zaidi baada ya mlimbwende huyo kujitokeza pamoja mwandaaji wa shindano hilo, Hasheem Lundenga kuzungumzia tuhuma zinazoendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Sitti alisema yeye ana umri wa miaka 23 na cheti chake cha kuzaliwa kilipotea kutokana na kusafiri mara kwa mara kwenda nje ya nchi hivyo kulazimika kuomba kingine. Hata hivyo hakusema kama aliwahikutoa taarifa polisi juu ya upotevu wa cheti chake.
Alipoulizwa juu ya uwepo wa hati ya kusafiria na leseni ya gari vinavyoenezwa mitandaoni vikionesha kwamba alizaliwa mwaka 1989 alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kina maana hakujiandaa kulizungumzia na pia ni masuala binafsi zaidi.
“…Sikutegemea haya maswali leo kwa hiyo sikuja nimejiandaa kihivyo, kama mtakua mnahitaji kunihoji mnaweza kupanga siku yenu na mkanihoji,” alisema. Mlimbwende huyo pia alikanusha vikali juu ya yeye kuwa na mtoto na kudai kinachofanyika ni uzushi wa baadhi ya watu katika mitandao ya jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashimu Lundenga akizungumza alisema wanachojua wao Sitti alikuwa na vigezo vya kushiriki shindano hilo kiumri kwani katika fomu alizotakiwa kujaza zinaonesha alizaliwa Mai 31, 1991 kwa hiyo alitimiza masharti ya kushiriki kwa kuwa alikuwa na umri usiopungua miaka 18 na usiozidi miaka 24.
“Wote walioshiriki Miss Tanzania 2014 akiwemo Sitti walituletea vyeti vyao Original vya kuzaliwa tarehe 13 na kisha tukatoa nakala kupitia hivyo vyeti…Sisi kazi yetu sio kupeleleza sana, tukipata ‘information’ chache zinatutosha…kama mtu anatatizo na hiki cheti cha Sitti cha kuzaliwa akafanye utafiti, ukipata ukweli tuletee sisi lakini kazi ya uchunguzi sio ya kwetu.’
“..Walidai kwamba Miss Tanzania ana mtoto baada ya kutoka picha akiwa na mtoto, nasema katika utafiti wetu sisi hana mtoto na mwenye vithibitisho halali kwamba ana mtoto atuletee, kama kuna uthibitisho wa cheti cha kuzaliwa cha mtoto…leta hicho cheti” alisema Lundenga.
Aidha akizungumzi madai ya kuwa waandaaji walipewa rushwa ili wamchague Sitti alisema tuhuma hizo ni za kijinga maana wanaosema hivyo hawajui namna majaji wa shindano hilo wanavyo patikana. Alisema majaji wa shindano hilo huteuliwa mwishoni kabisa jambo ambalo ni vigumu kumjua jaji na kumuhonga.
“Hili la sisi kuchukua rushwa kutoka kwa baba wa Sitti, Abbas Mtemvu…jamani hii ni stori ya kijingajinga, ni mambo ya kipumbavu sana kuandika haya, hamjui taratibu zetu tunavyowapata majaji na wanavyofanya kazi…majaji huwa wanatafutwa siku nne za mwisho na huwa hakuna mtu anajua atakua jaji na huwa tunapeleka majina 15 BASATA (Baraza la Sanaa Tanzania) na wao ndio wanaturudishia majina tisa ya Majaji waliopitishwa…,” alisema Lundenga.
Alifafanua kuwa kuhusu elimu ya Sitti wao hawana taarifa kuwa ana elimu ya masters kwa kuwa katika fomu alizojaza kwao hakusema hayo kama inavyoenezwa sasa. “Magazeti mbalimbali yameripoti kwamba Sitti alikua na masters, ukweli ni kwamba katika fomu tulizonazo sisi Sitti hajaandika hata sehemu moja kwamba amesoma mpaka masters, suala la masters limetoka wapi? Ni uwongo huo,’ alieleza mwenyekiti huyo wa Kamati ya Miss Tanzania.
“Kuhusu swala la yeye kuzungumza kifaransa, mtu anajua lugha ya kimataifa mbona kwenye mashindano ya dunia wanazungumza Kifaransa na lugha nyingine? lakini mbona hata kwenye fainali alijibu kwa Kiingereza pia? Kifaransa zilikua ni mbwembwe kuwashawishi Majaji, na kweli walishawishika na ndio maana akashinda,’ alibainisha Lundenga.