Misri kwachafuka; Mawaziri wajiuzulu

Machafuko yanayosababishwa na maandamanaji nchini Misri

BARAZA la mawaziri nchini Misri limeomba kujiuzulu kufuatia maandamano ya siku tatu mfululizo kupinga watawala wa kijeshi nchini humo, Televisheni ya Taifa nchini huo imeripoti.

Hata hivyo Msemaji wa Baraza la Mawaziri, Mohammed Hegazy amesema pamoja na uamuzi wao bado ombi lao la kujiuzulu halijakubaliwa na Baraza la Kijeshi linalotawala Misri. Wakati taarifa hizo zikitoka, maelfu ya waandamanaji wameendelea kufika katika viwanja vya Tahrir.

Hadi sasa zaidi ya watu 30 wameuwawa na wengine wapatao 1,800 kujeruhiwa kutokana na machafuko ya siku tatu yalioshuhudiwa katika mjini Cairo. Wakereketwa na waandamanaji wamekuwa wakilishinikiza baraza kuu la kijeshi linalotawala kukabidhi mamlaka kwa serikali ya kiraia.

Lakini hatua ya baraza la mawaziri la kutaka kujiuzulu huenda ikaitumbukiza nchi hiyo katika mzozo zaidi wa kisiasa. Tangazo la kutaka kujiuzulu litatafrisiwa kama ushindi kwa waandamanaji na huenda likawachochea kutoa matakwa zaidi.

Hii pia huenda ikalitatiza Baraza Kuu la Kijeshi, kwamba walirejeshe baraza hilo lililoomba kujiuzulu au wateuwe baraza jipya? lakini kwa vyovyote vile kutakuwa na shinikizo za kutaka serikali ya kiraia ipewe uwezo zaidi. Katika kipindi kizima cha maandamano, baraza hilo la kijeshi limekuwa likilaumiwa kwa kujipa madaraka makubwa.
-BBC