Kocha mkuu wa Timu ya Panone ya jijini Moshi FC Felix Minziro, siku chache mara baada ya kutua katika kikosi hicho kinachoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania Bara (FDL), Tayari ameanza kuunda kikosi upya kitakachoendana na kasi yake.
Msemaji wa timu hiyo Cassim Mwinyi alisema kuwa Minziro ameanza kazi yake ya kuunda kikosi kitakachoongeza nguvu katika mzunguko wa Pili wa ligi hiyo ambapo Panone Fc wataanza na JKT Oljoro wanaoongoza ligi hiyo kwa Pointi 14,katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
“kuna wachezaji 16 wameonesha nia ya kujiunga nasi na tayari Kocha amewajumuisha kwenye mazoezi ili mwisho wa siku ajue anaamchukua yupi na yupi amuache”
Kuna wachezaji wengi hapa wametoka timu ya Toto African, Mwadui, wengine Dar es salaam, na Zanzibar wote wanania ya kutaka kupata nafasi, hivyo hilo ni jukumu la Kocha kujua nani anafaa na si kuangalia ametoka wapi”aliongeza kusema Mwinyi.
Tayari Panone Fc katika kufanikisha adhma ya kupanda ligi kuu msimu ujao, wamemsaji Lusajo Mwakasagule ambaye aliwahi kuitumikia Klabu ya Yanga na Ruvu JKT kwa nyakati tofauti.
“tulikua na nafasi nne ikiwa na alama 11 za kusajili katika dirisha dogo la usajili na pia kuna wachezaji saba ambao mikataba yao imeisha, muda ukifika wote tutawaweka wazi waliotemwa na walioingia, hivyo tunafasi kumi za kusajili”alisema Mwinyi.
Kocha Minziro anachukua nafasi ya Atunga Manyundo ambaye ametemwa kwa kushindwa kufikisha malengo aliyojiwekee wakati akisaini mkataba, moja ikiwa ni kuiacha keleleni timu pindi mzunguko wa kwanza unapoisha lakini timu hiyo ipo nafasi ya tatu.