Na Janeth Mushi, Arusha
VIJANA wa Jumiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoani hapa, jana wameandamana hadi Kituo Kikuu cha Polisi kumsindikiza Mwenyekiti wa Umoja huo mkoani hapa, James Ole Millya ambaye alitakiwa kujisalimisha kwa Jeshi la polisi ili athibitishe kauli aliyoitoa dhidi ya jeshi hilo wakati wa mkutano ulioambatana na kuzinduliwa kwa matawi wilayani Arusha.
Aidha vijana hao waliandamana kuanzia majira ya saa 5:00 asubuhi kuanzia Makao Makuu ya UVCCM hadi Makao Makuu ya Polisi huku wakiwa katika makundi wakidai kuwa wamemsindikiza mwenyekiti wao na kutaka kujua hatama baada ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi.
Walipofika kituoni hapo, askari waliwazuia kuingia ndani ya geti kilipo kituo na kutakiwa kutawanyika kutokana na ufinyu wa eneo hilo ambapo walikaa pembeni kusubiri hatma ya Mwenyekiti wao, ambaye alifika eneo hilo majira ya saa sita mchana akiwa katika gari namba T457 AJV aina ya Landcruiser Lexus ameambatana na wakili wake, Mosses Mahunda.
Ole Millya akiongozana na wakili Mahunda pamoja na baadhi ya viongozi wa UVCCM na wazee walikwenda ofisi ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa ili kutii amri ya kutakiwa kujisalimisha lakini walipofika huko Mpwapwa aliomba afike leo kwani jana kulikuwa na shughuli za upokeaji mwenge na hivyo viongozi mbalimbali walikuwa huko, hivyo hivyo wasingeweza kumuhoji.
Baada ya maelezo hayo Millya na vijana wa Umoja huo walitoka wakitembea kwa miguu hadi ofisi za UVCCM Mkoa na kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo alidai kuwa mpaka sasa hajui anaitwa
kuhojiwa kwa ajili gani lakini kesho ndio atajua anahojiwa kwa sababu gani.
“Polisi ni sehemu salama sana na mtu yoyote anaweza kuitwa na kuhojiwa hivyo nasubiri nijue naitiwa nini mpaka sasa sijui naitwa kuhojiwa kwa sababu gani.”
Aidha Millya alizungumza na waandishi wahabari pamoja na vijana hao
nje ya ofisi za jengo la umoja huo ilikuwa imefungwa na kuwafanya
vijana waliokusanyika hapo kuhoji ni kwanini Mwenyekiti huyo azungumze nje ya ofisi tena ikiwa imefungwa wakati ni ofisi yake na alitakiwa kuzungumzia mambo ya chama akiwa ndani ya ofisi.
Aidha siku za hivi karibuni Jeshi la polisi mkoani hapa lilimtaka
Millya kufika Polisi kudhibitisha kauli yake aliyoitoa wiki
iliyopita kwenye shughuli za ufunguaji matawi zilizofanywa na
viongozi wa UVCCM ngazi ya Taifa na kutoa maneno kuwa kuna mtoto wa
kigogo ameshinikiza polisi kuzuia mkutano wao.
Kwa muji wa Mpwapwa alisema kuwa watamhoji Millya kuthibitisha kauli yake kuwa Jeshi hilo lilizuia mkutano wa CCM kutokana na na shinikizo la mtoto wa kigogo ambaye mpaka hivi sasa hajulikani.
Polisi walidai hawakuzuia mkutano huo bali Katibu wa UVCCM – Mkoa,
Abdallah Mpokwa alilitaarifu jeshi la polisi kwa simu kuwa mkutano huo umeahirishwa ila Oktoba 10 waliandamana bila kibali kwa kigezo cha kuwa wanafungua matawi ya wakereketwa, na kufanya maandamano yasiyo na kibali.