WATU watano wameuwawa na wengi zaidi ya 40 kujeruhiwa kwenye shambulio katika Kituo cha Basi cha Machakos mjini Nairobi, Kenya.
Taarifa zinasema kuwa maguruneti kama mane yalirushwa kutoka kwenye gari dhidi ya kituo cha basi cha Machakos Bus Station mjini Nairobi, ambacho kilikuwa kimejaa watu muda huo.
Shambulio hilo limetokea Jumamosi majira ya saa moja na nusu usiku. Hadi sasa inaarifiwa kuwa watu watano wamekufa, na wengi kujeruhiwa.
Mbunge wa jimbo hilo la Kamukunji, Yusuf Hassan, amesema amehesabu majeruhi wapatao 40 walipokuwa wakifikishwa hospitali ya taifa ya Kenyatta.
Bado haijajulikana nani amehusika katika shambulio hilo; wala kama washambuliaji ni wa ndani au kutoka nje ya nchi. Hassan alisema kuna majonzi na masikitiko mjini Nairobi kutokana na maafa hayo, lakini alisema safari za magari kwenye kituo zimeanza tena.
Aliwasifu watu wa Nairobu kuwa shupavu. Saa hizo za magharibi ni za harakati nyingi kwenye kituo hicho cha mabasi kutoka mikoani, na huwa na wasafiri wengi.
-BBC