Milioni 500 Zatengwa Ujenzi wa Nyumba za Walimu

Rais  Kikwete akihutubia

Rais Kikwete akihutubia

Serikali imetenga Shilingi Milioni Mia Tano (Tshs 500m) kwa Halmashauri 41 nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora za Walimu.

Rais Jakaya Mrisho Kikwete amewaambia Wananchi wa Tanga, 27 Machi,2014 wakati akihutubia Mkutano wa hadhara katika barabara ya Karume kuwa;

“Tayari Halmashauri za Mkinga, Pangani na Kilindi zimeshapata pesa hizo , na tumetenga kiasi kama hicho kwa kila Halmashauri zingine nchini ili kuboresha makazi na Nyumba za Walimu ” Rais amesema.

Fedha hizo ni sehemu ya fedha iliyotengwa maalum na Serikali kwa ajili ya kujenga nyumba za walimu katika Halmashauri arobaini na moja (41) nchini kote katika kipindi cha Mwaka wa fedha wa 2013/14.

Halmashauri zingine zitakazofaidika na mpango huo ni Mlele, Nsimbo , Meatu, Makete, Ngorongoro na Longido. Pia Halmashauri za Bagamoyo, Mafia, Kisarawe, Rufiji,, Kigoma, Kasulu, Kibondo, Nachingwea, Kilwa, Liwale,Ruangwa Rorya, Chunya, Ileje, Rungwe, Kilombero, Ulanga, Newala, Tandahimba na Nanyumbu zitafaidika na mpango huo wa Serikali.

Aidha, Halmashauri za Ukerewe, Sengerema, Kwimba, Tunduru, Namtumbo na Sikonge pia zimo katika mpango huo wa Mwaka huu wa fedha.

Halmashauri za Muleba, Ngara, Nkasi, Kiteto na Simanjiro nazo zimo katika mpango huu ambao Serikali imedhamiria kuutekeleza ili hatimaye kuwatengenezea mazingira mazuri walimu hapa nchini.

Rais amemaliza awamu ya kwanza ya ziara yake ya kikazi Mkoani Tanga ambapo ametembelea, kukagua shughuli za maendeleo na kufungua miradi ya Barabara, Maji, Soko na Maabara Mkoani Tanga.

Katika ziara yake hiyo Rais ametembelea Wilaya za Handeni, Korogwe, Muheza na Tanga ambapo katika awamu ya pili Rais amepanga kutembelea Mkinga, Lushoto, Kilindi na Pangani.