JUMLA ya watoto 20,500 inadaiwa hawajapewa chanjo kati ya mwaka 2009 hadi 2011 huku wazazi wengi wakionekana kukumbatia mila potofu kuwa chanjo ina madhara kwa watoto. Katika hali ya kukwepa huduma za chanjo wazazi wengi wakijifungulia nyumbani na kutowapeleka watoto hospitalini kupewa huduma ya chanjo.
Takwimu hizo zimetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alipokuwa akizindua wiki ya chanjo duniani kimkoa ilifanyika wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akitoa takwimu zaidi, Mulongo alisema kwa mwaka 2009 watoto 6,313 hawakupewa chanjo, mwaka 2010 watoto 8,271 huku mwaka 2011 watoto 5,666 hawakupatiwa chanjo kabisa. Alisema hali hiyo ni hatari kwani inasababisha milipuko ya magonjwa mbalimbali ikiwemo surua.
Mulongo ameagiza sekta ya afya Mkoa wa Arusha kubeba jukumu hilo na kuhakikisha ifikapo mwaka 2015 kusiwe na mototo ambaye hajapatiwa chanjo. Malengo ya wiki ya chanjo ni kuhamasisha watoto wanaostahili kupatiwa chanjo na wale ambao hawajakamilisha kupata chanjo wanapatiwa chanjo kwa kupelekwa katika vituo vya afya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa. Dk. Frida Mokiti, alisema
chanjo za watoto zilikuwa zinatolewa wiki nne mara mototo anapozaliwa, ila kutokana na dunia kutoa chanjo hizo wiki sita na Tanzania sasa itatoa wiki sita ili kuwe na usawa.
Dk. Mokiti alisema Mkoa wa Arusha kwa sasa ugonjwa unaoongoza kuuwa watoto wadogo ni Nimonia, badala ya Malaria kama ilivyokuwa hapo awali, ambao umeshika nafasi ya tatu hii ni kutokana na kugawiwa
vyandarua.
“Wazazi nawahimiza mhakikishe mnawapeleka watoto wenu katika vituo vya afya wapatiwe chanjo, ili kuweza kuwakinga na magonjwa yanayozuilika kwa kupata chanjo,” alisema Dk. Mokiti.